WAANDISHI WA HABARI WAKIWA KWENYE KONGAMANO LILILOANDALIWA NA MISA-TAN
Na Rose Mweko
KONGAMANO la MISA Tanzania lililofanyika jijini Mwanza limewakutanisha wahariri, waandishi wa habari na wadau kutoka taasisi mbalimbali za Serikali na sekta binafsi, kwa lengo la kujenga mahusiano yenye tija kati ya tasnia ya habari na wadau wa maendeleo nchini.
Kongamano hilo lilihudhuriwa na wanachama zaidi ya 60 wa MISA Tanzania kutoka Kanda ya Ziwa, Kanda ya Magharibi na Kanda ya Kati, pamoja na wawakilishi wa taasisi mbalimbali zikiwemo Idara ya Uhamiaji, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) na taasisi nyingine.
MWENYEKITI WA MISA-TAN TAWI LA TANZANIA EDWIN SOKO
Akifungua kongamano hilo, Mwenyekiti wa MISA Tanzania, Edwin Soko, alisema chama hicho kinatambua umuhimu wa wadau kutoka sekta mbalimbali kutokana na mchango wao katika kukuza na kuendeleza tasnia ya habari.
Soko alisema ushiriki wa wadau hao ni muhimu katika kujenga uelewa wa pamoja, kuimarisha mawasiliano na kuweka mazingira yatakayowawezesha wanahabari kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Alieleza kuwa majukwaa ya aina hiyo yanatoa fursa kwa wanahabari na wadau kujadiliana, kubadilishana uzoefu na kujenga uhusiano mzuri katika masuala yanayohusu maendeleo ya jamii.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Daniel Machunda, aliyewasilisha salamu kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, aliipongeza MISA Tanzania kwa kuandaa kongamano hilo na kuwakutanisha wadau wa sekta mbalimbali.
Machunda aliwataka waandishi wa habari kutumia taaluma yao kuibua na kuhabarisha umma kuhusu fursa mbalimbali za maendeleo zilizopo katika jamii, ili wananchi waweze kuzitambua na kuzitumia kujiletea maendeleo.
Alisisitiza kuwa vyombo vya habari vina nafasi muhimu katika kuelimisha jamii, kusambaza taarifa sahihi na kuhamasisha wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo.
Kongamano hilo limekuwa jukwaa la wanachama wa MISA Tanzania na wadau mbalimbali kubadilishana mawazo na kujadili namna ya kukuza tasnia ya habari na kuimarisha mchango wake katika maendeleo ya nchi.








0 Maoni