Marie Msellemu, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa TPDC.

Na RoseMweko, Geita

SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limesema linaendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha rasilimali za mafuta na gesi nchini zinatumika ipasavyo kwa manufaa ya Watanzania na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.


Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa TPDC, Marie Msellemu, wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Geita katika semina iliyolenga kuwapa uelewa kuhusu shughuli za shirika hilo, matumizi ya gesi asilia pamoja na nafasi ya sekta ya mafuta na gesi katika uchumi wa Taifa.


Semina hiyo iliyofanyika jana, Septemba 3, 2026, katika Ukumbi wa Harvest Hotel, Geita mjini, iliwakutanisha waandishi wa habari kutoka mkoani humo kwa lengo la kuwawezesha kupata taarifa sahihi na za kina kuhusu sekta hiyo, ili waweze kuwafikishia wananchi elimu kuhusu fursa zinazopatikana.


Msellemu alisema TPDC inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia maslahi mapana ya Taifa, ikiwamo kuhakikisha rasilimali za petroli zinatumika katika kuongeza thamani ya uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.


Aidha, semina hiyo ilitoa nafasi kwa washiriki kupata taarifa kuhusu maendeleo ya Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda.


Kaimu Mratibu wa Mradi wa EACOP kutoka TPDC, Jumanne Mohammed Said, alieleza hatua mbalimbali zilizofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo, huku akibainisha umuhimu wake katika kukuza uchumi wa Tanzania na kuimarisha nafasi ya nchi katika sekta ya nishati katika ukanda wa Afrika Mashariki.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Geita, Renatus Masuguliko, alisema ni muhimu waandishi wa habari kupata taarifa sahihi kutoka kwa wataalamu na taasisi zinazohusika na sekta ya mafuta na gesi.


Masuguliko alisema uelewa huo utawawezesha wanahabari kuandika habari zenye usahihi na kuwasaidia wananchi kufahamu fursa, manufaa na mchango wa sekta ya mafuta na gesi katika maendeleo ya Taifa.


Alisema ushirikiano wa karibu kati ya TPDC na vyombo vya habari ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata elimu sahihi kuhusu shughuli zinazotekelezwa katika sekta hiyo, badala ya kutegemea taarifa zisizo na uhakika.



Semina hiyo imekuwa sehemu ya jitihada za kuimarisha uhusiano kati ya TPDC na waandishi wa habari, huku msisitizo ukiwekwa katika umuhimu wa vyombo vya habari kushiriki kikamilifu katika kuelimisha umma kuhusu rasilimali za mafuta na gesi na mchango wake katika uchumi wa Tanzania.