NA ROSE MWEKO,GEITA.
Mkuu mpya wa Mkoa wa Geita, Alexander Mnyeti, amewatahadharisha watendaji wa Serikali mkoani humo kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na kwa kuzingatia kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, akisisitiza kuwa hatavumilia uzembe, uzururaji kazini wala tabia ya mtendaji yeyote anayekwamisha maendeleo ya wananchi.
Mnyeti alitoa kauli hiyo mara baada ya kuwasili rasmi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, ambako alipokelewa kwa heshima na shangwe na wafanyakazi wa Sekretarieti ya Mkoa pamoja na watendaji mbalimbali. Alisema nafasi za uongozi ni dhamana kubwa inayopaswa kutumiwa kwa kuwatumikia wananchi na kuhakikisha maelekezo ya Serikali yanatekelezwa kwa wakati na kwa ufanisi.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa aliahidi kufanya kazi kwa karibu na watendaji wote wa Mkoa wa Geita, akisema mafanikio ya Serikali hayawezi kupatikana kwa mtu mmoja bali yanahitaji ushirikiano, mshikamano na uwajibikaji wa kila mmoja. Alisisitiza kuwa atakuwa tayari kusikiliza ushauri kutoka kwa watendaji na wadau mbalimbali ili kuboresha utendaji na kuongeza kasi ya maendeleo.
Mnyeti pia aliwataka watendaji kuwa na mtazamo wa kutatua changamoto badala ya kuwa sehemu ya matatizo, huku akisisitiza umuhimu wa kusimamia rasilimali za umma kwa uaminifu na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora. Alisema hatasita kuchukua hatua pale atakapobaini uzembe au mtendaji anayefanya kazi kwa namna inayokwamisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Serikali.
Akiwahakikishia watumishi ushirikiano, Mnyeti alisema ujio wake Geita unaenda sambamba na dhamira ya kuimarisha utendaji, kusukuma mbele miradi ya maendeleo na kuhakikisha wananchi wananufaika na juhudi za Serikali. Aliwataka watendaji kujiandaa kufanya kazi kwa kasi, ubunifu na uwajibikaji, akisisitiza kuwa Geita inahitaji watumishi wanaochapa kazi na si wanaosubiri kusukumwa ili kutekeleza majukumu yao.





0 Maoni