Na Rose Mweko
Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), kwa kushirikiana na Waandishi wa Habari za Pamba na Mazingira (TACOEJ), imeendesha mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari kutoka mikoa mitano, yakilenga kuwajengea uwezo wa kuandika na kuripoti habari za zao la pamba kwa usahihi na weledi.
Mafunzo hayo yaliyofanyika Agosti 17, 2026 katika Ukumbi wa Bodi ya Pamba Tanzania mjini Shinyanga, yamewapa waandishi uelewa kuhusu sekta ya pamba, changamoto zinazowakabili wakulima, hatua zinazochukuliwa na Serikali pamoja na namna vyombo vya habari vinavyoweza kuchangia kuongeza tija na ubora wa zao hilo.
Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba Kanda ya Magharibi, Afisa Kilimo wa Bodi hiyo, Penina Range, amewataka waandishi kuzingatia weledi, usahihi na taaluma katika kuandika na kuripoti habari zinazohusu pamba.
Amesema waandishi wanapaswa kutumia taarifa sahihi kutoka vyanzo vinavyoaminika ili kuhakikisha wakulima wanapata elimu inayoweza kuwasaidia kuongeza uzalishaji na tija.
«“Kupitia mafunzo haya mkawe mabalozi wa kuelimisha wakulima ili kuongeza tija ya uzalishaji wa pamba. Wakulima wengi wanahitaji elimu sahihi kutoka kwa waandishi wa habari. Andikeni kwa usahihi, weledi na kuzingatia taaluma zenu,” amesema Penina.»
Penina pia amewataka waandishi kujenga utamaduni wa kuwasiliana na Bodi ya Pamba wanapokuwa na mashaka kuhusu taarifa wanayotaka kuchapisha au kutangaza, ili kupata ufafanuzi kutoka kwa wataalamu.
WAANDISHI WANA MCHANGO MKUBWA KATIKA SEKTA YA PAMBA
Akizungumza katika mafunzo hayo, Afisa Kilimo na Uhamasishaji wa Zao la Pamba, Edward Nyawile, amesema waandishi wa habari wana nafasi kubwa katika maendeleo ya sekta hiyo kutokana na uwezo wao wa kufikisha taarifa na elimu kwa wakulima na wadau wengi kwa wakati mmoja.
Nyawile amesema zao la pamba linasimamiwa chini ya Sheria ya Pamba Na. 2 ya mwaka 2001, huku Serikali kupitia Bodi ya Pamba ikiendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuongeza uzalishaji na tija kwa wakulima.
Amesema Bodi ya Pamba imenunua matrekta 680 kwa ajili ya kurahisisha shughuli za kilimo na kupunguza utegemezi wa jembe la mkono.
Aidha, amesema Bodi imeanza kusajili wakulima katika mfumo wa kidijitali kwa lengo la kuwa na kanzidata itakayosaidia katika kupanga na kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo ya zao la pamba.
Nyawile pia amesema maandalizi yamefanyika kwa ajili ya kuanzishwa kwa ekari 1,000 za kongani za viwanda katika eneo la Misungwi, hatua inayolenga kuongeza thamani ya zao hilo na kuchochea uchakataji na shughuli za viwanda.
USAFI NA UBORA WA PAMBA WAPEWA KIPAUMBELE
Akitoa mada kuhusu usafi na ubora wa pamba, Afisa Kilimo anayeshughulikia upande wa Maabara kutoka Bodi ya Pamba, Doto Ntumba, amesema Tanzania ina maabara moja ya usanifu wa pamba iliyopo Shinyanga, ambayo pia inahudumia nchi za Kenya na Uganda.
Amesema bado kuna changamoto ya uchafuzi wa pamba wakati wa uvunaji, uhifadhi na usafirishaji, jambo linaloweza kuathiri ubora na thamani ya zao hilo katika soko.
Doto amesema maabara hiyo ina vitengo vya usanifu wa pamba kwa kutumia mikono na mashine, ambapo wataalamu hupokea sampuli za pamba, kufanya uchunguzi na kutoa madaraja ya ubora.
Amesisitiza kuwa elimu kwa wakulima ni muhimu katika kuhakikisha Tanzania inazalisha pamba safi na yenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko.
PAMBA INALIMWA KATIKA MIKOA 17
Kwa upande wake, Katibu wa TACOEJ, Sitta Tuma, amesema mafunzo hayo yatawasaidia waandishi kuwa na uelewa mpana wa sekta ya pamba na hivyo kuandika habari zenye usahihi na manufaa kwa wakulima.
Amesema pamba inalimwa katika mikoa 17 nchini, hivyo ni muhimu kwa waandishi wanaoripoti kutoka maeneo hayo kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu sekta hiyo.
Amesema TACOEJ itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuwajengea uwezo waandishi wa habari ili kutumia taaluma yao kuelimisha jamii na kuchochea uzalishaji wenye tija.
WAKULIMA WAHITAJI ELIMU ZAIDI
Naye Mwandishi wa Habari na Mtangazaji kutoka Faraja FM, Moshi Ndugulile, amesema mafunzo hayo yamewapa waandishi uelewa utakaowawezesha kuripoti masuala ya pamba kwa kina na kuzingatia mahitaji halisi ya wakulima.
Amesema wakulima wanahitaji elimu zaidi kuhusu kanuni bora za kilimo, uvunaji, uhifadhi na utunzaji wa pamba ili kuongeza uzalishaji na ubora.
Ndugulile amesema waandishi wanapaswa kutumia nafasi yao kuibua changamoto zinazowakabili wakulima, kutoa elimu sahihi na kuonyesha fursa zilizopo katika sekta ya pamba.
Amesema pamba imewahi kuitwa “Dhahabu Nyeupe” kutokana na umuhimu wake kiuchumi, hivyo juhudi za pamoja za Serikali, wakulima, wadau wa sekta na vyombo vya habari zinahitajika kuongeza tija, ubora na thamani ya zao hilo.
Mafunzo hayo yamewakutanisha waandishi wa habari kutoka mikoa inayozalisha pamba, ambapo wamepata fursa ya kujifunza masuala mbalimbali kuhusu uzalishaji, usafi na ubora wa pamba, sera na sheria zinazosimamia zao hilo pamoja na nafasi ya vyombo vya habari katika kuelimisha na kuhamasisha wakulima.










0 Maoni