Afisa Elimu Msingi Halmashauri ya wilaya ya Geita Paul Magubiki.
Tukio la kushtua limeripotiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita, ambapo Afisa Elimu wa wilaya hiyo, anayejulikana kwa jina la Paul Magubiki, anadaiwa kumshambulia hadharani aliyekuwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Katoma, Mohamed Waziri, kabla ya kumteka na kutokomea naye kusikojulikana.
Inasemekana, tukio hilo lilitokea mwezi Novemba, majira ya saa tatu asubuhi, wakati wa mitihani ya taifa ya darasa la pili. Inadaiwa kuwa Afisa Elimu huyo alimvamia mwalimu mbele ya watu na kumpiga makofi, hali iliyosababisha taharuki miongoni mwa walimu na wanafunzi waliokuwepo.
Baada ya tukio hilo, mwalimu alitekwa na kuondolewa eneo la shule, huku akinyang’anywa simu yake ya mkononi, ambayo ilishikiliwa kwa muda wa siku tatu. Hadi sasa, mazingira ya kutoweka kwake kwa muda huo hayajawekwa wazi kikamilifu.
Mwandishi wa habari alifanya juhudi za kumtafuta mwalimu Waziri, akizungumza kwa masikitiko, Mohamed Waziri alisema tukio hilo limemuathiri kwa kiasi kikubwa kisaikolojia, akieleza kuwa amekuwa akiishi kwa hofu na msongo wa mawazo tangu litokee.
“Nimeathirika sana kiakili na kihisia. Ni jambo ambalo sikuwahi kufikiria lingeweza kunitokea katika mazingira ya kazi,” alieleza.
Baada ya kurejeshewa uhuru wake, mwalimu huyo aliendelea kukumbwa na vitisho, ambavyo vilifuatiwa na uamuzi wa kuhamishwa kutoka Shule ya Msingi Katoma kwenda Shule ya Msingi Sozibuye, iliyopo jimbo la Busanda bila kupata stahiki zake za uhamisho.
Kwa sasa, Mohamed Waziri alisema ameanza kufuata taratibu za kisheria na kiutumishi ili kudai haki yake. Tayari amewasilisha malalamiko rasmi kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita pamoja na Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, akitaka uchunguzi wa kina ufanyike na hatua zichukuliwe dhidi ya waliohusika.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya Geita Daudi Mlahagwa alisema ni kweli tukio hilo lipo na tayari amemuagiza afisa utumishi utumishi kulichunguza kwa undani ili kupata undani wake.
" ni kweli tumepokea barua ya malalamiko ya Mwalimu Waziri na tayari nimemuagiza afisa utumishi kulifuatilia ili kutoa maamuzi sahihi" alisema Mlahagwa.
The Profile ilimtafuta afisa elimu huyo ambapo alisema hajui kama kuna tukio hilo hivyo hawezi kuongelea tukio ambalo halitambui.
" ninashangaa sana hizi tuhuma mimi sizijui kabisa sasa kama ninalalamikiwa ntaitwa na mkuu wangu ndie nitakayemjibu" alisema Magubiki.
wadau wa elimu na haki za binadamu wameziomba mamlaka husika kuchunguza suala hilo kwa haraka na haki itendeke.
Tukio hili limeibua maswali mazito kuhusu usalama wa walimu kazini na matumizi ya madaraka katika sekta ya elimu.



0 Maoni