KAMANDA WA POLISI MKOA WA GEITA SACP SAFIA JONGO AKIWA ENEO LA MGODI WA MSASA
JESHI la Polisi mkoani Geita limethibitisha kuwa hakuna madhara ya binadamu yaliyotokana na ajali ya kutitia maduara manne ya uchimbaji madini katika Mgodi wa Msasa wilayani Bukombe mkoani Geita.
Tukio hilo lilitokea Machi 29, 2026 majira ya saa nne asubuhi katika eneo la maduara ya uchimbaji yanayofanyiwa ukarabati katika mgodi huo ulipo kata ya Runzewe Magharibi.
Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Safia Jongo ametoa taarifa hiyo mara baada ya jeshi la zimamoto la uokoaji kukamisha zoezi la uchunguzi.
Shughuli za uokozi zikiwa zinaendelea eneo lililotitia Msasa
Kamanda Jongo amesema uchunguzi umebainisha kuwa wakati wa tukio hilo hakuna shughuli za uchimbaji zilizokuwa zinaendelea kwa sababu tahadhari ilishatolewa baada ya kutiliwa mashaka.
“Tulifanya juhudi kwa kushirikiana na uongozi wa mgodi, kuhakikisha kwamba tunalifukua lile eneo lote ambalo limetitia ili kujiridhisha kwamba hakuna madhara yoyote yaliyotokea”.
Amesema baada ya zoezi la ufukuaji kukamilika baadhi ya mali zinazotumika kwenye shughuli za uchimbaji zilikutwa chini lakini hakukuwa na mwili ama viashiria vya binadamu chini ya aridhi.
“Uvumi uliotokea ni mkubwa sana, kwamba watu zaidi ya 200, lakini nathibitisha kwamba mgodi huu kweli umetitia lakini hakuna madhara kwa binadhamu yaliyotokea.
“Naomba nitoe wito kwa jamii kuacha kutoa taarifa za uzushi pale ambapo changamoto inapotokea, na niwaombe wale waliofanya hivo watoe taarifa zao kwenye mitandao", amesema Kamanda Jongo.
Kamanda Jongo amesema kwa yeyote atakayekiuka maelekezo ya jeshi la polisi na kuendelea kusambaza taarifa za uongo hatua za haraka zitachukuliwa ili kudhibiti upotoshaji na taharuki.
“Mkoa wa Geita kwa ujumla wake ni salama, na mgodi wa Msasa kwa ujumla wake ni salama, na changamoto zilizotokea ni kawaida kwenye shughuli za uchimbaji”, amesema Kamanda Jongo.
Amesema tahadhari, maelekezo na mafunzo ya kiusalama yameshatolewa kwenye maeneo yote ya wachimbaji wadogo katika msimu huu wa mvua za masika ili kuepuka madhira zaidi.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Geita, Keneth Mwakasitu amesema uchunguzi na ufuatiliaji katika eneo la tukio umefanyika kwa weledi kubaini madhara ya ajali.
Mwakasitu amesema hadi kufikia majira ya saa mbili usiku hakuna madhara ya binadamu yaliyobainika kupitia mazoezi ya utafutaji na uokoaji yaliyotekelezwa katika eneo hilo.
“Kazi imekuwa rahisi, kazi imekuwa nzuri, na uzushi wowote unaoendelea kwenye habari za mtandaoni ni uongo, hakuna madhara yoyote yaliyotokea katika huu mgodi”, amesema.
MWISHO





0 Maoni