DKT FRED MSEMWA AKIPOKELEWA OFISI YA MSAJILI WA HAZINA TAIFA
Na Rose Mweko, Dar es Salaam
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Uwekezaji, Dkt. Fred Msemwa, amepongeza mabadiliko chanya yanayoendelea katika Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH), akisema yanachochea maendeleo ya uchumi wa Taifa.
Akizungumza na wafanyakazi wa ofisi ya msajili wa Hazina wakati wa ziara yake ya kujitambulisha baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Dkt Msemwa alisema kumekuwepo na juhudi kubwa ya kuhakikisha ofisi ya hazina inakua kisasa na inaendana na kasi ya ukuaji wa kiuchumi.
Dkt. Msemwa alifahamishwa kuhusu muundo wa taasisi, majukumu yake, utekelezaji wa mipango ya maendeleo, na mafanikio yaliyopatikana katika usimamizi wa uwekezaji wa Serikali.
Katika kikao cha pamoja na menejimenti ya OMH, Dkt. Msemwa alipokea wasilisho la kina kuhusu shughuli za taasisi hiyo na mchango wake katika kuongeza mapato ya Serikali na kuimarisha nidhamu ya matumizi ya rasilimali za umma aidha kuongeza tija katika uwekezaji wa umma.
Dkt Msemwa alisisitiza kuwa usimamizi madhubuti wa rasilimali za umma, uwazi, na uwajibikaji ni misingi muhimu katika kujenga uchumi imara na endelevu.
“Ofisi ya Msajili wa Hazina imeonyesha mafanikio makubwa katika kuboresha utendaji na mageuzi yake, na ninashukuru kwa juhudi za kuimarisha mchango wa taasisi za umma katika uchumi wa taifa. Ni lazima tuchukue hatua madhubuti katika kuhakikisha kwamba rasilimali za umma zinatumika kwa ufanisi na uwazi,” alisema Dkt. Msemwa.
Dkt. Msemwa aliahidi kutoa ushirikiano kwa wote ili kutatua changamoto yoyote inayoweza kuathiri utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo, akisisitiza umuhimu wa kazi ya pamoja ili kuongeza ufanisi katika usimamizi wa uwekezaji wa Serikali.
Kwa upande wake, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, alimshukuru Dkt. Msemwa kwa kutembelea ofisi hiyo na kwa kuonyesha nia ya kuimarisha mshikamano na mawasiliano kati ya taasisi hizo.
Alisisitiza kwamba ushirikiano wa karibu kati ya Ofisi ya Rais Uwekezaji na Ofisi ya Msajili wa Hazina utaongeza ufanisi wa usimamizi wa uwekezaji wa Serikali na kulinda maslahi ya Taifa.
“Ziara hii ni hatua muhimu ya kuimarisha ushirikiano wetu na Ofisi ya Rais Uwekezaji. Tunahitaji kuwa na taasisi imara zinazozingatia matokeo ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu yetu kwa ufanisi. Ushirikiano huu utahakikisha tunafikia malengo yetu ya maendeleo,” alieleza Bw. Mchechu.
Ziara ya Dkt. Msemwa inatoa fursa ya kuimarisha mahusiano ya kikazi kati ya ofisi hizo mbili, huku ikijenga msingi wa ushirikiano wa kimkakati utakaosaidia kuongeza tija, uwazi, na mchango wa taasisi za umma katika maendeleo ya kiuchumi ya Tanzania.






0 Maoni