Naibu Waziri wa TAMISEMI anayeshughulikia masuala ya afya, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Busanda, Dkt. Jafari Rajabu Seif, ametoa wito kwa watumishi wa afya kote nchini kuhakikisha wanatumia lugha ya upole, staha na tabasamu wanapotoa huduma kwa wagonjwa wanaofika katika vituo na zahanati za serikali.
Dkt. Jafari alitoa kauli hiyo wakati wa ziara ya kushtukiza aliyofanya katika Kituo cha Afya cha Nyarugusu kilichopo katika Kata ya Nyarugusu, Jimbo la Busanda, Wilaya ya Geita.
“Serikali ya Dkt. Samia itaendelea kuboresha huduma za afya, ikiwemo ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya vituo vya afya na zahanati. Hata hivyo, pamoja na maboresho hayo, nyinyi watoa huduma mna wajibu wa kumpokea mgonjwa kwa tabasamu na kutumia lugha safi, si lugha chafu,” alisema Dkt. Jafari.
Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mfawidhi wa kituo hicho Fredi Feliasianj alisema kuwa wamefurahishwa na ziara ya Naibu Waziri, kwani kituo hicho kinahudumia wananchi wengi na kinahitaji maboresho makubwa ili kuendelea kutoa huduma bora kwa jamii.






0 Maoni