MAMLAKA ya Mapato Nchini (TRA) imewataka watanzania kuzingatia mabadiliko ya taarifa za umiliki wanapouza magari ili kuwezesha mabadiliko ya taarifa za mlipa kodi na kuepusha changamoto zingine.
Aidha TRA imetahadharisha kuwa iwapo mabadiliko ya taarifa za umiliki hayatafanyika kwa wakati na kwa ufasaha na gari hiyo ikatumika kinyume cha sheria muuzaji atakuwa ndio mtuhumiwa wa kosa hilo.
Ofisa Elimu na Mawasiliano wa TRA mkoa wa Kagera, Rwekeza Rwegoshora amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Viwanja vya Maonyesho ya Teknolojia ya Madini mjini Geita.
Rwekeza amesema watu wengi wamekuwa wakifanya mauziano ya magari kwa mazoea na bila kubadili taarifa za mlipakodi hali ambayo imeifanya TRA kushindwa kupata taarifa za mmiliki mpya kwa wakati.
“Mauziano haya yamekuwa yakifanyika kwa mazoea, watu hawajui athari, anachukua chombo chake cha moto, wanauziana bila kubadili umiliki”, amesema.
Aidha amewatahadharisha watanzania kutambua endapo taarifa za mmiliki na mlipa kodi wa chombo cha moto zisipobadilishwa na ikatumika kwenye shughuli za uharifu inaweza kumtia kwenye hatia muuzaji.
“Kwa sababu za kiusalama ni vyema sasa wakabadilisha umiliki ukakamilika kabla ya kukabidhiana hivyo vyombo vya moto”, amesema Ruekeza.
Alisema pia TRA imeendelea kusisitiza msamaha wa rib ana adhabu kwa magari ambayo yameingia nchini bila kufuata utaratibu wa forodha ambapo kikomo chake ni Desemba 31, 2025” amesema.
Amesema TRA pia imewahimiza wafanyabiashara wa mtandao kujisajili ili nao waweze kulipa kodi kama wafanyabiashara wengine na mwitikio umeonekana.
MWISHO
0 Maoni