Afisa Mkuu wa Kodi kutoka Kitengo cha Elimu na Mawasiliano wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Geita, Bw. Justin Katiti akifafanua jambo 

Geita, Tanzania Wafanyabiashara mkoani Geita wametakiwa kuhakikisha wanatumia Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) katika shughuli zao zote za kibiashara ili kuhakikisha wanalipa kodi kwa mujibu wa sheria na kuchangia maendeleo ya taifa.

Rai hiyo imetolewa na Afisa Mkuu wa Kodi kutoka Kitengo cha Elimu na Mawasiliano wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Geita, Bw. Justin Katiti, wakati wa maonesho ya nane ya teknolojia ya madini yanayoendelea mkoani Geita, alipotembelewa na Mkuu wa Wilaya ya Geita Bw Hasim Komba aliotembelea banda la TRA katika viwanja vya maonesho.



Bw. Katiti amesema kuwa matumizi ya TIN ni ya lazima kwa kila mfanyabiashara, na kwamba kutokuwa na TIN au kutotumia namba hiyo katika miamala ya biashara ni kinyume cha sheria za kodi. Amesisitiza kuwa TIN huisaidia TRA kufuatilia kwa ufanisi ulipaji wa kodi, lakini pia humsaidia mfanyabiashara kujitambulisha kisheria na kupata huduma mbalimbali kutoka taasisi za kifedha na kiserikali.

 “Mfanyabiashara yeyote anapaswa kuwa na TIN na kuitumia katika shughuli zake za kibiashara. TIN si tu kwa ajili ya kulipa kodi, bali pia ni utambulisho muhimu unaomwezesha mfanyabiashara kushiriki kikamilifu katika mfumo rasmi wa uchumi,” alisema Katiti.

Aidha, amewahimiza wafanyabiashara wadogo na wa kati ambao bado hawajasajiliwa, kufika katika banda la TRA kwenye maonesho au ofisi yoyote ya mamlaka hiyo ili kupata usajili wa TIN bure pamoja na elimu ya kodi.


Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mheshimiwa Hashim Komba, amewahamasisha wananchi wa Geita na mikoa ya jirani kufika kwa wingi kwenye maonesho hayo ya teknolojia ya madini, ambayo ni jukwaa muhimu kwa wadau mbalimbali kujifunza, kupata huduma na kuonesha ubunifu katika sekta ya madini na biashara.

“Maonesho haya ni fursa ya kipekee kwa wananchi na wafanyabiashara kupata maarifa, huduma na kujionea teknolojia mbalimbali zinazotumika katika sekta ya madini. Nawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kutembelea mabanda, ikiwemo banda la TRA, ili kunufaika na elimu ya kodi na huduma nyingine muhimu,” alisema DC Komba.



Maonesho ya nane ya teknolojia ya madini yamekusanya taasisi mbalimbali za serikali na binafsi, wajasiriamali, wachimbaji, na wadau wa maendeleo, yakiwa na lengo la kuhamasisha matumizi ya teknolojia, uwajibikaji wa kifedha, na ushirikiano katika kuendeleza rasilimali za madini nchini.