Maofisa wa Tanesco wakitoa ufafanuzi wa matumizi ya nishati ya umeme ya kupikia kwa wadau mbalimbali.

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoa wa Geita limetoa uhakika wa huduma ya umeme wa kutosha kwa watumiaji wa vifaa vya umeme majumbani na viwandani kutokana na uwepo wa umeme unaotosheleza mahitaji.

Meneja wa Tanesco mkoa wa Geita, Joachim Ruweta ametoa kauli hiyo katika akiwa katika viwanja vya Dk Samia Suluhu yanapofanyika Maonyesho ya Nane ya Teknolojia ya Madini mjini Geita.

Maofisa wa Tanesco wakitoa ufafanuzi wa matumizi ya nishati ya umeme ya kupikia kwa wadau mbalimbali.

Amesema kutokana na uhakika wa huduma ya umeme wa kutosha hivo wananchi wote wasiogope kutumia aina zote za vifaa vya umeme ikiwemo pasi, majiko, mashine za kufulia kwani huduma ni ya uhakika.

Joackimu amesema kwa mlengo huo wananchi wa Geita wanayo nafasi ya kuunga mkono matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kununua majiko ya umeme kwani Unit moja inaweza kupika kwa saa moja.

Amesema tahadhari kubwa ya kuzingatiwa ni mifumo ya umeme ndani ya nyumba inapaswa kuunganishwa na watalaamu kutoka Tanesco ili kuepuka ajali ya moto unaoweza kutokana na shoti ya umeme.

Amesema mpaka sasa Geita ina kituo kikubwa cha kufua na kupoza umeme chenye uwezo wa kuzalisha Megawati 90 ambazo zinatosheleza kabisa kukidhi mahitaji ya kijamii, kiuchumi kwa wakazi wa Geita.

Kwa Upande wake Ofisa Huduma kwa Wateja Tanesco Geita, Aveline Christian amesisitiza kuwa majiko ya umeme yamethibitishwa na hayawezi kusababisha ajali ya shoti ya umeme kwa urahisi.

Mkuu wa wilaya ya Geita, Hashimu Komba amesema kuwa hatua hiyo ni mwendelezo wa serikali kuhamasisha wananchi waweze kuachana na matumizi ya kuni na mkaa na kutumia nishati safi zaidi.

Amesema kwa wilaya ya Geita mpaka sasa vijiji 155 kati ya vijiji vyote 158 sawa na asiimia 98 vimeshafikiwa na umeme na hivo kutoa uwanja mpana kwa wakazi wa Geita kutumia umeme katika uchumi wao.

“Vijiji vitatu vilivyobaki vipo katika kisiwa cha Izumacheli ambapo Tanesco wanaendelea na kazi ya kupeleka umeme kupitia mfumo wa umeme jua.


“Tunapoona jiko la umeme lenye uwezo wa kupika lisaa limoja kwa uniti moja ni ishara kwamba taasisi na jamii wameielewa vyema dhana ya Dk Samia kwenye eneo la matumizi ya nishati safi ya kupikia”, amesema.