BODI ya Maziwa Nchini (TDB) imefanikiwa kufikisha programu ya unywaji wa maziwa kitaifa katika shule 218 sambamba na kuwafikia wanafunzi 122,481 ambao wamepatiwa elimu na huduma ya maziwa.
Aidha TDB kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imefanikiwa kufikia mikoa 11 ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha unywaji wa maziwa mashuleni ili kuinua afya ya mwili na akili ya wanafunzi.
Mwakilishi wa Msajili TDB, Deorinidei Mng'ong'o alieleza hayo jana katika hafla ya maadhimisho ya siku ya unywaji wa maziwa kitaifa iliyofanyika katika Viwanja vya Dk Samia Bombambili mjini Geita.
Alisema kwa kitaalamu inashauriwa kila mmoja kunywa angalau glasi moja ya maziwa kila siku ili kutengeneza mazingira endelevu ya ukua kimwili na kiakili.
“Dhumuni la program ya unywaji wa maziwa mashuleni ni kupunguza hali ya udumavu, kwani udumavu usipochukuliwa hatua mapema huenda likawa ni tatizo la kudumu kwa mtoto.
“Tukimuwahi mapema huyu mtoto tutakuwa na uhakika wa kutengeneza kizazi kijacho kilicho na vijana wenye akili na uwezo wa kupambanua mambo na kuhakikisha taifa la vijana lenye kuleta maendeleo”.
Mratibu wa Shirika la Land’O Lakes, Joackimu Balakana alisema lengo la kuwekeza elimu ya unywaji wa maziwa shuleni ni kuwafanya watoto wawe mabalozi wa kampeni hiyo katika jamii.
Mwakilishi wa mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la Heifer International, Nyamate Musobi alisema kampeni ya unywaji maziwa shuleni imekuwa na mafanikio makubwa nyanda za juu kusini na kufikia watoto 16,000.
“Tunaendelea kutoa rai tuweze kuona mkoa wa Geita, Tanzania nzima, miradi kama hii inazaa matunda hivo tushirikiane kwa pamoja ili tuweze kuleta mapinduzi” alisema Musobi.
Mwakilishi wa mkuu wa mkoa wa Geita, Mkuu wa wilaya ya Geita, Hashimu Komba aliagiza shule, taasisi na wadau wa maendeleo kuungana kwa pamoja kuleta matokeo chanya ya unywaji wa maziwa shuleni.
0 Maoni