Kigoma Kaskazini,
NA ROSE MWEKO
Kampeni za uchaguzi wa ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) zimezinduliwa rasmi kwa kishindo katika kijiji cha Mahembe, ambapo mgombea ubunge Peter Serukamba alitangaza rasmi nia yake ya kuendelea kulitumikia Jimbo la Kigoma Kaskazini kwa kipindi kingine cha miaka mitano.
Katika tukio lililovutia maelfu ya wakazi wa Mahembe na maeneo jirani, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Mheshimiwa John Mongela, aliongoza uzinduzi huo kwa hotuba iliyosisitiza umuhimu wa kuendeleza uongozi wa kiongozi mwenye ufanisi, uzoefu na uthubutu wa kweli wa kuleta maendeleo.
WANANCHI WALIOJITOKEZA KATIKA UZINDUZI
Akizungumza na wananchi, Mongela alisema Serukamba ana historia ya kutekeleza, si kuahidi tu.
Alisema amekuwa kiungo muhimu wa maendeleo katika Kigoma Kaskazini na sasa ni wakati wa kumrudisha ili akamilishe alichoanza. Aliongeza kuwa wanamtuma Serukamba kwa kazi, si kwa maigizo ya kisiasa.
"Nimerudi Kukamilisha Tulichoanza Pamoja ikiwemo Ujenzi na ukarabati wa barabara za vijijini, upatikanaji wa huduma bora za afya na Maji safi na salama aidha uwezeshaji wa vijana kupitia mafunzo ya ufundi na ajira
Serukamba alisema anafahamu changamoto za wananchi wa Mahembe na vijiji vingine vya Kigoma Kaskazini,
"Hawa ni ndugu zangu nimeishi nao, nimewasikiliza, na sasa ni wakati wa hatua zaidi".
Alisema kazi aliyokwishaianza itakamilishwa kwa pamoja na wananchi.
Uzinduzi huo uliambatana na burudani za asili, nyimbo za kampeni, na kauli mbiu zenye ushawishi mkubwa. Wananchi walionyesha imani yao kwa Serukamba kwa kumpokea kwa shangwe na vigelegele, huku wakimuelezea kama kiongozi anayewasikiliza na kuchukua hatua.
Mzee Rashid Athumani, mkazi wa Mahembe, alisema Serukamba si mtu wa majukwaani tu, bali ni mtu wa vitendo.
"Tumemuona akileta maji, shule na barabara, hivyo hawana sababu ya kubadili dereva wakati safari inaendelea vizuri".
MWISHO







0 Maoni