Mkuu wa Wilaya ya Geita (DC), Mhe. Hashim Komba, ametoa wito kwa taasisi za usimamizi wa sekta ya fedha kuhakikisha zinasimamia hadi kwenye taasisi ndogo za wananchi (Vicoba) ili kuepuka hasara ambazo zinatokea kutokana na kukosa usimamizi Madhubuti.


Mkuu huyo wa wilaya ameyasema hayo wakati alipotembelea banda la Bodi ya Bima ya Amana (DIB) katika Maonesho ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika viwanja ya Dkt. Samia Suluhu Hassan Bombambili mjini Geita.


“Tumekuwa tukipata malalamiko kutoka kwa wananchi ambao wamejiwekea hisa zao katika Vicoba hala pengine mmojawapo anatoroka na fedha na inakuwa kazi ya kumtafuta,” Bw. Komba na kutaka taasisi za udhibiti kuhakikisha kwamba wanafika hadi huko ili kuleta utulivu.

Ameitaka DIB kushirikiana na BoT na taasisi nyingine za usimamizi kuhakikisha kwamba usimamizi Madhubuti unafika hadi kwenye ngazi za Vicoba ili kuondoa sintofahamu zinazojitokeza katika vikundi hivyo.

Bw. Komba ameipongeza Bodi ya Bima ya Amana kwa kazi zake ambazo alisema zinaongeza imani ya wananchi katika kutumia huduma za kifedha zinazotolewa na benki na taasisi za fedha.


Alisema kuwa na uhakika kwamba mtu akiwa na akaunti yake benki, halafu benki ikafungwa au kufilisika anaweza kupata fedha zake ni jambo jema sana.

Mapema Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Umma na Mawasiliano wa DIB, Bw. Lwaga Mwambande, alimweleza Mkuu huyo wa Wilaya kwamba Bodi ya Bima ya Amana inakinga amana za wananchi katika benki na taasisi za fedha dhidi ya hasara ambayo inaweza kutokea endapo taasisi kama hizo zitafungwa au kufilisika.


Tofauti na bima nyingine, wachangiaji katika Mfuko wa Bima ya Amana ambao unasimamia na DIB ni benki na taasisi za fedha zenye leseni ya Benki, wakati wateja wa benki na taasisi za fedha hizo ni wanufaika tu wa fidia endapo benki ikifilisika.

Majukumu mengine ya Bodi ya Bima ya Amana ni kuendesha zoezi la ufilisi wa benki au taasisi ya fedha endapo ikiteuliwa na Benki Kuu ya Tanzania pamoja kupunguza hasara kwa benki au taasisi ya fedha ambayo inapitia changamoto zinazotishia usalama wake.

Kwa mujibu wa uzoefu, jukumu la kuhusika na kupunguza hasara (Loss Minimiser) linasaidia siyo tu kunusuru benki zisife au kufilisika, bali pia linaweza kuwa la gharama nafuu kuliko zoezi la fidia na ufilisi baada ya benki kushindwa kufanya kazi, mtawali.