NA ROSE MWEKO, GEITA.

Mgombea ubunge wa Jimbo la Busanda, Wilaya ya Geita kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Jafari Rajabu Seif, amezindua rasmi kampeni zake kwa kuahidi kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi na kuhakikisha Busanda inapata maendeleo ya kweli.


Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika katika shule ya msingi Nyarugusu, iliyopo Kata ya Nyarugusu, Dkt. Jafari aliwaomba wananchi wamchague kwa kura nyingi ili aweze kuwatumikia kwa ufanisi.


"Ilani ya CCM imeeleza mengi, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara ya kutoka hapa Nyarugusu kwenda hospitali ya wilaya. Ninawaahidi ndugu zangu, nitasimamia kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kikamilifu," alisema Dkt. Jafari.


Aliongeza kuwa lengo lake ni kuhakikisha Jimbo la Busanda linapiga hatua kubwa kimaendeleo kwa kushirikiana na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kutoka Mkoa wa Geita, Elivalist Gervas, aliwahimiza wananchi wa Busanda kumuunga mkono Rais Dkt. Samia, pamoja na kuwapigia kura za kishindo wagombea wa CCM 

 kuanzia ngazi ya ubunge hadi udiwani  katika uchaguzi utakaofanyika Oktoba 29.