Naibu Mkuu wa Takukuru mkoa wa Geita, Alex Mpemba
Na Rose Mweko , Geita.
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Geita imebaini dosari kwenye upande wa matumizi ya fedha katika miradi miwili yenye thamani ya sh milioni 917.72.
Miradi hiyo ni miongoni mwa miradi 29 ya maendeleo yenye thamani ya sh bilioni 9.5 iliyochunguzwa na kufanyiwa ufuatiliaji na Takukuru mkoani humo kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2025.
Naibu Mkuu wa Takukuru mkoa wa Geita, Alex Mpemba alibainisha hayo jana mbele ya waandishi wa habari alipowasilisha taarifa ya utendaji wa Takukuru kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita.
Mpemba alisema tayari uchunguzi umeanzishwa kubaini mnyororo mzima wa watu waliohusika kwenye dosari ya malipo ya fedha hizo ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.
Aliongeza pia Takukuru imefanikiwa kudhibiti ufujaji wa kiasi cha sh milioni 14.2 pamoja na kufanikisha kupatikana kwa sh milioni 3.2 zilizolipwa na mwekezaji wa kijiji.
"Fedha hizo (milioni 14) zimeokolewa katika miradi minneya elimu ambayo ilibainika baadhi ya wazabuni kulipwa kinyume cha mkataba, malipo ya bidhaa pungufu na dhaifu.
"Pia kulikuwa na mabadiliko ya kazi yasiyoendana na mabadiliko ya gharama mradi, mafundi kulipwa kabla ya kazi kufanyika na kutokuwasilishwa kwa kodi ya zuio serikalini", alieleza Mpemba.
Alisema kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba 2025, Takukuru inaendelea kupokea na kufanyia kazi taarifa za watia nia ili kudhibiti mienendo michafu inayoweza kupelekea matumizi ya rushwa katika uchaguzi.
"Tehama sasa hivi ipo vizuri, wananchi wanatoa taarifa vizuri, tumekuwa tukiingilia na kuzia zaidi vitendo hivo, tunachotaka sisi watu wafuate utaratibu", alisisitiza Mpemba.
MWISHO
0 Maoni