MWENEZI WILAYA YA GEITA AFUNGUKA MAFANIKIO YA ILANI YA 2020/2025
Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa ambaye pia ni Katibu wa Siasa na Uenezi wa Wilaya ya Geita, Gabriel Nyasunga Nyasilu, amesema Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015/2020 imetekelezwa kwa kiwango kikubwa, hasa katika sekta muhimu kama elimu, afya, miundombinu ya barabara, maji, na nishati ya umeme.
Akizungumza leo katika viwanja vya ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Nyasilu amesema utekelezaji wa miradi hiyo umechochea maendeleo ya wananchi na kuinua hali za maisha, hasa kupitia mikopo mbalimbali inayotolewa na serikali kwa ajili ya kuwawezesha kiuchumi.
"Serikali kupitia Ilani ya CCM imejipambanua kwa kutekeleza miradi yenye tija kwa wananchi. Tumeshuhudia maendeleo makubwa, hususan katika kutoa huduma za kijamii na kuwawezesha wananchi kushiriki katika uchumi wa taifa," alisema Nyasilu.
Aidha, alibainisha kuwa chama kinajipanga kutoa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2025/2030, ambayo itakuwa na mwelekeo wa kutatua changamoto zinazowakabili Watanzania na kugusa maeneo yote muhimu yanayohitaji maboresho.
"Ilani ijayo itakuwa ya matumaini mapya, tukilenga kuendeleza mafanikio yaliyopatikana na kufungua fursa zaidi kwa wananchi," aliongeza.
0 Maoni