Na Rose Mweko, Kigoma
Katika mfumo wa kisiasa wa Tanzania,
wanawake wameendelea kupiga hatua kubwa katika uongozi, licha ya changamoto
nyingi zinazowakabili. Mgeni Omary, Diwani wa Kata ya Kipampa, na Naibu Meya wa
Manispaa ya Kigoma/Ujiji, ni miongoni mwa wanawake shupavu wanaoonyesha uwezo
wa wanawake katika uongozi wa kisiasa.
Bi Mgeni Omary Kakolwa alianza
uongozi kama mjumbe Serikali ya mtaa wa Lutare 2004-2009 ambapo kwa mafaniko
aliyoyapata aliweza kuwa diwani vitimaalum 2010-2020 ambapo baada ya mafanikio
ya uongozi katika Nyanja zote hizo Mgeni Omary mwaka 2020 alifanikiwa kugombea
udiwani kata ya Kipampa katika kipindi chote cha uongozi wake ameonyesha
uthabiti na ujasiri katika utumishi wake huku akiwa taa na kilelezo kwa
wanawake wa Kata ya Kipampana Mji wa Kigoma kwa ujumla.
Aidha Mgeni Amefanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali
ya maendeleo ikiwemo uboreshaji wa
huduma za kijamii ambapo ametumia uzoefu wa uongozi kuhimiza ujenzi wa
miundombinu bora kama shule, zahanati, na barabara zinazorahisisha usafiri kwa
wananchi aidha amekuwa mstari wa mbele
kuwahamasisha ushiriki wanawake katika maendeleo kwa kusimamia
uanzishwaji wa vikundi vya wanawake kwa lengo la kuwawezesha kiuchumi kupitia
mikopo na mafunzo ya ujasiriamali.
Pia Bi
Mgeni amekuwa kiongozi mwenye ushirikiano na jamii yake ambapo amejenga mahusiano mazuri kati ya serikali za
mitaa na wananchi huku akisisitiza uwazi na uwajibikaji kwa viongozi na
watendaji ili kuhakikisha wananchi wanapata haki zao bila kubugudhiwa hii
imemfanya kuwa kiongozi anayependwa na wananchi wake.
Kwa upande wa Naibu Meya wa Manispaa
ya Kigoma/Ujiji, ameleta mchango mkubwa katika kuimarisha utawala wa kidemokrasia kwa kusimamia vikao vya
halmashauri kwa haki na usawa, kuhakikisha sauti ya kila mmoja inasikika, aidha
amekuwa mstari wa mbele kupigania
maendeleo ya wanawake ambapo amekuwa akihamasisha wanawake wengi
kushiriki katika siasa na kujihusisha na shughuli za maendeleo, aidha Bi Mgeni ameweza kuimarisha usafi wa
mazingira na huduma za jamii
Kupitia sera zake, amesimamia usimamizi bora wa taka na kuimarisha
upatikanaji wa maji safi.
Ushiriki wa wanawake katika siasa
una athari chanya kwa jamii kwa njia mbalimbali ikiwemo kuimarisha maendeleo ya jamii kwani wanawake wanapokuwa sehemu ya
maamuzi ya kisiasa, wanahakikisha kuwa masuala yanayowahusu wanawake na watoto
yanapewa kipaumbele, kama vile elimu, afya, na ustawi wa familia.
Aidha
mwanamke anaongeza Kuchochea uwajibikaji na uwazi
kwani Tafiti zinaonyesha kuwa wanawake viongozi mara nyingi wanahimiza uwazi na
uwajibikaji katika utawala, hali inayosaidia kupunguza rushwa na matumizi mabaya
ya madaraka huku wakisaidia kuvunja
vikwazo vya kijinsia kwa Wanawake wanaoshiriki katika siasa kwani
wanakuwa mfano wa kuigwa kwa kizazi kipya cha wasichana, wakionyesha kuwa
uongozi sio wa wanaume pekee.
Hivyo
ushiriki wa wanawake katika siasa huleta usawa wa kijinsia na huimarisha uwakilishi wa kijinsia katika vyombo vya
maamuzi na kuhakikisha kuwa sauti za wote zinajumuishwa katika sera na maamuzi
ya kitaifa na hivyo kuongeza mshikamano
wa kijamii kwani wanawake wanasiasa mara nyingi hujikita katika
kuimarisha mahusiano ya kijamii na kutatua migogoro kwa njia ya amani, hali
inayosaidia kujenga jamii yenye mshikamano na utulivu.
Kumekuwepo na jitihada mbalimbali kimataifa kuhakikisha kunakuwepo na
usawa katika uongozi ambapo baadhi ya mikataba ya kutokomeza ubaguzi kimataifa
imefikiwa ikiwemo Mkataba wa kutokomeza aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake
(CEDAW) – 1979 ulipitishwa na Umoja wa Mataifa (UN) mwaka 1979 na
kuanza kutumika mwaka 1981 ndani ya mkataba huo unasisitiza haki za wanawake
kushiriki kikamilifu katika maisha ya kisiasa na ya umma (Kifungu cha 7 na 8)
aidha unazihimiza nchi wanachama kuchukua hatua za kuhakikisha uwiano wa
kijinsia katika ngazi za maamuzi.
Aidha
kumekuwepo na maazimio na matamko mengi katika kuhakikisha wanawake wanafikia
haki yao katika harakati hizo kumekuwepo na azimio maarufu duniani kama Azimio la Beijing (Beijing Declaration and Platform
for Action) – 1995 ambapo katika azimio hilo lilipitishwa
katika Mkutano wa nne wa wanawake wa umoja wa mataifa, miongoni mwa maazimio
hayo ni pamoja na kuwa azimio linasisitiza usawa wa kijinsia katika uongozi wa
kisiasa na wa kitaasisi aidha inapendekeza sera za kuwezesha uwakilishi wa
angalau 50/50 katika siasa na uamuzi wa umma.
Katika mipango mbalimbali ya kimataifa suala la haki sawa kijinsia
limepewa kipaumbele ambapo katika Malengo ya Maendeleo Endelevu (Sustainable
Development Goals – SDGs) – 2015 lengo namba 5 la SDGs linahimiza
usawa wa kijinsia, likilenga kushirikisha wanawake kikamilifu katika uongozi,katika
kipengele cha 5.5 kinazitaka nchi kuhakikisha fursa sawa kwa wanawake katika
maamuzi ya kisiasa, kiuchumi, na umma.
Mikataba
ya kimataifa ya kuhakikisha usawa wa kijinsia katika ngazi za uongozi ni mingi Mkataba wa Maputo (The
Maputo Protocol) – 2003 ni mkataba wa umoja wa Afrika (AU)
kuhusu haki za wanawake barani Afrika, unasisitiza usawa wa kijinsia katika
siasa na maamuzi ya umma (Kifungu cha 9) aidha Mkataba wa SADC juu ya jinsia na maendeleo –
2008 ulipitishwa na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
(SADC),ambapo unazitaka nchi wanachama kufanikisha uwakilishi wa 50/50 katika
nafasi za uamuzi ifikapo 2030.
Hata hivyo, utekelezaji wa kanuni ya 50/50
bado unakumbwa na changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na mifumo ya kisiasa, mila
na desturi, na ukosefu wa sheria za kitaifa zinazounga mkono kikamilifu usawa
wa kijinsia.
Sheria za kimataifa kuhusu uwakilishi wa
kijinsia wa 50/50 katika ngazi za maamuzi zinatokana na mikataba, maazimio, na
makubaliano mbalimbali ya kimataifa kwani hakuna sheria moja ya kimataifa
inayotamka moja kwa moja kanuni ya 50/50, lakini kuna nyaraka na makubaliano
yanayosisitiza usawa wa kijinsia katika uongozi na maamuzi.
Tanzania ina sheria na sera kadhaa
zinazohakikisha usawa wa kijinsia katika ngazi za maamuzi. Ingawa hakuna sheria
moja inayotamka moja kwa moja uwiano wa 50/50, kuna nyaraka na sheria
zinazosisitiza ushirikishwaji wa wanawake katika uongozi wa kisiasa na maamuzi.
Baadhi ya sheria hizo ni pamoja na katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977, marekebisho mbalimbali).
Ibara
ya 13(1) na (2) Inasisitiza usawa wa watu wote mbele ya sheria bila
ubaguzi wa kijinsia, aidha Ibara ya
66(1)(b) na 78(1) Inatambua
nafasi za viti maalum kwa wanawake katika Bunge ili kuhakikisha ushiriki wao
katika maamuzi ya kitaifa huku Ibara ya
9(h) Inalenga kuhakikisha kuwa wanawake wanashiriki kikamilifu katika
shughuli za taifa.
Aidha Sheria ya Uchaguzi (1985, marekebisho
mbalimbali) Inatoa nafasi kwa wanawake kushiriki
kwenye chaguzi za kisiasa kwa kuweka utaratibu wa viti maalum ili kuongeza
uwakilishi wao katika Bunge na mabaraza ya mitaa, huku sheria ya Serikali za Mitaa (1982, marekebisho mbalimbali) inasisitiza
usawa wa kijinsia katika nafasi za uongozi kwenye serikali za mitaa, pia inahakikisha
kuwa wanawake wanashiriki katika mabaraza ya madiwani na maamuzi ya maendeleo
ya jamii.
Kwa ujumla, sheria hizi zimechangia
kuongezeka kwa idadi ya wanawake katika ngazi za maamuzi nchini Tanzania,
lakini bado kuna changamoto za utekelezaji, ikiwa ni pamoja na mifumo ya
kijamii na kisiasa inayoweza kuzuia uwiano wa kijinsia katika uongozi.
Pamoja na kuwepo sheria na maazimio
mbalimbali ya kuhakikisha wanawake wanapewa kipaumbele katika uongozi bado kuna
changamoto wanazokumbana nazo wanawake katika
siasa, wanawake katika siasa za Tanzania bado wanakabiliwa na changamoto
kadhaa, ikiwa ni pamoja na ufinyu wa
fursa za kifedha.
Wanawake wengi hukosa rasilimali za kifedha za
kuendesha kampeni zao na kushindana na wagombea wa kiume wenye mtaji mkubwa
hivyo kukata tamaa aidha sababu nyingne ni ukosefu wa usaidizi wa kijamii na familia kwani majukumu ya kifamilia mara nyingi huwa kikwazo
kwa wanawake kushiriki kikamilifu katika siasa.
Aidha vikwazo
vya kijamii na kiutamaduni, mila na
desturi katika jamii nyingi bado zinapendelea wanaume kushika nafasi za
uongozi, hali inayopunguza uungwaji mkono kwa wanawake kwani kumekuwepo na
vitendo vya unyanyapaa na vitisho vya
kisiasa kwa baadhi ya wanawake kwani hukumbana na matusi, kejeli, na
hata vitisho vinavyolenga kuwakatisha tamaa katika safari yao ya kisiasa.
Hivyo basi
kumekuwepo na uwakilishi mdogo katika vyama vya siasa licha ya juhudi mbalimbali bado idadi ya wanawake katika
vyama vya siasa na nafasi za maamuzi bado ni ndogo ikilinganishwa na wanaume.
Hivyo basi Wanawake kama Mgeni Omary
Kakolwa Diwani wa kata ya Kipampa na Naibu Meya wa Kigoma/Ujiji wanaendelea
kuwa mfano wa kuigwa kwa wanawake wengine wanaotamani kushiriki katika siasa.
Ingawa changamoto bado zipo, mafanikio yao yanaonyesha kuwa kwa kupewa nafasi
wanawake wanaweza kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
Ni muhimu kwa jamii, serikali, na
taasisi za kiraia kuendelea kushinikiza usawa wa kijinsia katika siasa kwa
kutoa fursa zaidi kwa wanawake kushiriki na kushikilia nafasi za uongozi kwani
demokrasia yenye uwakilishi sawa wa jinsia zote huleta maendeleo jumuishi na
kuimarisha ustawi wa jamii kwa ujumla.
0 Maoni