Na Rose Mweko, Geita
SERIKALI imewataka watanzania kuwa na nidhamu ya fedha, kukopa kwa ajili ya mahitaji yenye tija na kuchukua mikopo kwa ajili ya shughuli za uzalishaji mali ili kuepukana na janga la mikopo umiza.
Aidha imeiagiza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na ofisi zote zinazoshughulika na usimamizi wa sekta ya fedha na Kamati zote za Ulinzi na Usalama kufuatilia kwa ukaribu taasisi zote zinazotoa mikopo nchini.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Stansilaus Nyongo ametoa maelekezo hayo alipomwakilisha Waziri wa Fedha katika uzinduzi wa jengo la Ofisi za Hazina Ndogo mkoa wa Geita.
Nyongo amesema changamoto ya mikopo umiza imekuwa ni ya muda mrefu na inaendelea kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi wa kawaida hivo ni lazima hatua zichukuliwe haraka kukomesha tatizo.
"Naelekeza kuchukua hatua kali dhidi ya wanaotoa huduma za fedha bila leseni na kuwanyanganya leseni wote watakaobainika wanatoa mikopo bila kuzingatia mashariti ya leseni.
"Natoa onyo kwa watu binafsi na kampuni zinazojihusisha na utoaji wa mikopo ya namna hii kuacha mara moja kwani jambo hili linarudisha nyuma wananchi wetu kiuchumi", amesema Nyongo.
Amesema uwepo wa ofisi za hazina ndogo mkoa wa Geita itawapunguzia wananchi kutembea umbali mrefu na gharama ili kupata huduma pamoja na kuwasaidia kupata elimu ya kifedha kutoka kwa watumishi wa hazina.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Lasius Mwenda amesema jingo lina ofisi 14 zitakazotumika na watumishi 50 na litatumiwa na Idara mbili ambazo ni Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali na Hazina Ndogo mkoa wa Geita pamoja na Ofisi ya Takwimu mkoa wa Geita.
“Jengo hili litaboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wetu, na wateja wetu, itapunguza gharama za uendeshaji wa ofisi hususani kukodi kwa maana ya kulipa pango", amesema Mwenda.
Mshauri Elekezi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Amina Lumuli amesema mradi wa Jengo la Hazina Ndogo Geita umetekelezwa na Mkandarasi Masasi Construction Ltd. Co pamoja na TBA ambaye ni mshauri elekezi.
“Mradi ulianza Juni 30, 2023 na kukabidhiwa Desemba 03, 2024 ambapo mradi huu ni wa miezi 15, gharama za mradi ni sh bilioni 4.37 pamoja na VAT gharama za mshaur elekezi ni sh milioni 269", amesema.
Mwakilishi wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na Mbunge wa Meatu, Leah Komanya amesema serikali itaendelea kuiwezesha ofisi ya mweka hazina ili kutoa mafunzo kwa wahasibu wa ofisi ndogo za hazina.
Amesema lengo la kuwajengea uwezo wahasibu ni kuondoa chanagmoto kubwa ya uandaaji wa taarifa na usimamizi wa fedha za serikali za mitaa zinzotolewa na serikali kuu na kupunguza ukiritimba.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mkuu wa wilaya ya Geita, Hashimu Komba amesema uwepo wa ofisi ndogo za hazina Geita itaondoa usumbufu kwa wananchi kufuata huduma za hazina mkoani Mwanza.
MWISHO
0 Maoni