Diwani Kata ya Kakubilo Kesi Gayo Nyanda akiwa na mwenyekiti wa Jumuia ya wazazi Wilaya ya Geita na mwenyekiti wa UWT wilaya ya Geita
Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Geita imepongeza hatua ya Diwani wa Kata ya Kakubilo, Kesi Gayo Nyanda, kwa kutoa eneo lake lenye hekari sita kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Msingi Ikigilo, iliyopo katika Kijiji cha Kikwete, Kata ya Kakubilo.
Pongezi hizo zilitolewa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Geita, Barnabas Mapande, wakati wa ziara ya kukagua mradi wa ujenzi wa shule hiyo akiwa ameambatana na Kamati ya Siasa.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Geita Barnabas Muhoja Mapande
Akitoa taarifa kuhusu maendeleo ya ujenzi huo, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Leonard Lukas, alisema kuwa serikali imepanga shilingi milioni 351 kupitia mradi wa BOOST kwa ajili ya ujenzi wa madarasa saba, ikiwemo mawili maalumu kwa elimu ya wanafunzi wenye mahitaji maalum. Ujenzi huo ulianza Juni 2024 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Januari 2025.
Hatua ya Diwani Nyanda imetajwa kuwa mfano wa kuigwa kwa viongozi wengine katika kuchangia maendeleo ya jamii, hususan sekta ya elimu.
0 Maoni