MKUU WA MKOA GEITA AKITETA JAMBO NA MHANDISI DEUSDEDITH MALULU KUTOKA REA

MKOA WA GEITA WAUPOKEA MRADI WA MAJIKO YA GESI 16,275 KUTOKA REA*

*Kila wilaya imetengewa mgao wa majiko 3,255*

Mkuu wa mkoa wa Geita, Mhe. Martine Shigela, tarehe 02 Desemba, 2024 amepokea majiko ya gesi 16,275 yenye thamani ya shilingi milioni 285 katika hafla ya iliyofanyika kwenye Ofisi ya Mkuu wa mkoa na kutoa wito kwa Wananchi kuendela kuhamasisha Wananchi kuchangamkia fursa ya nishati safi ya kupikia.



Mhe. Shigela amesema majiko hayo ya gesi yamekuja kama sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia uliozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mwezi Mei mwaka huu na kusisitiza kuwa safari ya kubadili fikra za wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi inapaswa kuungwa mkono na Wadau wengi.


“Tunawashukuru REA kwa kutuletea mitungi (Majiko ya gesi) mengi kwa ajili ya kuwapa Wananchi wa mkoa wa Geita kwa bei ya ruzuku, maelekezo ya Serikali ni kuhakikisha mitungi hii (Majiko ya gesi) inakwenda kuwasaidia Wananchi walio vijijini na itakwenda kwa Wananchi wetu walio kwenye Halmashauri zetu sita (6) na haitaishia kwenye makao makuu ya wilaya, itakwenda kwenye kata na vijiji”. Amesema Mhe. Shigela.

MHANDISI DEUSDEDITH MALULU AKIFAFANUA JAMBO


Kwa upande wake, Mhandisi Mwandamizi Msimamizi wa Miradi kutoka REA, Deusdedith Malulu amesema fursa ya kupata jiko la gesi la kilo sita (6) ni kwa kila Mwananchi na kuongeza kuwa sharti la kupata jiko hilo ni Kitambulisho cha Taifa au namba ya NIDA pamoja shilingi 17,500 amezitaja wilaya zinazonufaika na Mradi huo ni pamoja na wilaya ya Geita, Bukombe, Chato, Mbogwe na Nyang’hwale.


“Kila wilaya, itapelekewa majiko ya gesi 3,255 pamoja na vichomeo vyake (Burners) kupitia kampuni MANJIS Logistic Ltd. Tunaendelea kuhamasisha kuhusu matumizi ya nishati safi ili wajitokeze kwa wingi kununua mitungi hii, inayotolewa kwa bei ya punguzo ya asilimia 50,” ameeleza, Mhandisi, Malulu.

MKUU WA MKOA GEITA MARTINE SHIGELA


Wakati huo huo, Mhandisi Malulu amemueleza Mkuu wa mkoa Geita kuwa REA imeleta fursa ya mkopo na nufuu wa ujenzi wa vituo vidogo vya bidhaa za mafuta vijijini yaani (Diseli na Petroli) ambapo kila Mwananchi mwenye nia ya kutaka kujenga kituo kidogo cha mafuta vijijini anaweza kuomba mkopo wenye riba nafuu pamoja na ukomo wa miaka saba na kuongeza kuwa shilingi milioni 133 zinakopeshwa kwa ajili ya ujenzi wa kituo kimoja cha mafuta.


Mhandisi Malulu ameongeza kuwa masharti ya kupata mkopo huo ni nafuu na kwamba masharti ya mkopo huo pamoja fomu za maombi, zinapatikana kwenye tovuti ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa anwani ya [www.rea.go.tz]



MWISHO!