JE DEMOKRASIA YA SIASA TANZANIA INAMTAMBUA
MWANAMKE KWA KIWANGO GANI.
*Leo tunaangazia Wanawake na Demokrasia Changamoto na Fursa
"UKATILI wa Kijinsia na kisaikolojia bado
ni tatizo kubwa kwenye siasa kwa kuwa bado wanawake walioamua kuingia kwenye
ulingo huo wanapitia udhalilishaji na shinikizo la jamii kuachana na nafasi
wanazogembea kwa kuwa ni kwa ajili ya wanaume,"ndivyo anavyoanza kueleza
Diwani wa Viti Maalum Manispaa ya Kigoma Ujiji, Mashavu Barakabise.
Anasema hali hiyo inatokana na mtazamo wa
kihistoria unaochukulia wanawake kama wasiofaa katika nyanja za uongozi, na
mara nyingi huwafanya wanawake kuwa na hofu ya kujitokeza kugombea nafasi za
kisiasa.
Mashavu anasema miaka ya nyuma ilikua ngumu
kuwapata wanawake kushirikii katika siasa kutokana na mtazamo hasi wa jamii
kuwa wanawake waliopo kwenye siasa hawana maadili na hii ilitokana na kwamba
kwa wakati huo mwanamke alikuwa hawezi kusimama na kuchangia hoja za maendeleo
katikati ya wanaume ikichukuliwa kama utovu wa nidhamu ambapo waliitwa majina
dhalili kama jikedume na mengineyo mengu hivyo kwa miaka ya zamani iliwawia
ugumu sana kuwahamasisha wanawake kujitokeza japo walijitokeza kwa uchache
tofauti na ilivyo sasa ambapo sasa elimu imewafikia jamii na kuwawezesha kuona
kila mtu anastahili kuchangia katika harakati za maendeleo ya jamii.
Kwa mujibu wa Taasisi ya Kimataifa ya Demokrasia
(NDI), katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2020 wanawake waliochaguliwa kwa nafasi za
ubunge ni asilimia 9.5, wabunge wa viti maalum ni asilimia 29, hivyo kufanya
jumla ya wabunge 142 kati ya 393.
Vilevile, Ripoti ya Tume Huru ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) ya mwaka 2020 inaonesha wanawake waliochaguzliwa kwa nafasi za
udiwani walikuwa asilimia 6.58, viti maalum walikuwa 1,374 katika halmashauri
184 sawa na asilimia 24.59.Kwa ujumla wanawake walikuwa asilimia 29.24 ya
madiwani wote nchi nzima.
Aidha, Ripoti ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
Mwaka 2019 pia inaonesha kuwa kati ya nafasi 11,915 za wenyeviti wa vijiji,
wanawake walishinda nafasi 246 sawa na asilimia 2.1 huku wanaume wakishika
asilimia 97.9 ya nafasi hizo. Kati ya nafasi 4,171 za wenyeviti wa mitaa,
wanawake walishinda nafasi 528 sawa naasilimia 12.6.
Pia Ripoti ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ya mwaka 2023 inaonesha kuwapo ongezeko kubwa la udhalilishaji wa kidijitali na ukatili wa kijinsia mtandaoni nchini, wanawake wakiwa walengwa wakuu kwa asilimia 56.
Wakati ripoti mbalimbali zikionesha hayo, Mashavu anasema bado uwakilsihi wa wanawake kwenye vyama vya siasa ni mdogo huku ajenda na ilani za vyama zikipuuzia maslahi ya wanawake katika uwanja wa siasa, hali anayoona inafanya mchakato wa kisiasa kutokuwa rafiki kwa wanawake.
Diwani Mashavu ni miongoni mwa viongozi wanawake waliochaguliwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 akitokea Kata ya Majengo Manispaa ya Kigoma Ujiji, ambaye anasema wakati naingia kwenye uwanja wa siasa dhamira yake ilikuwa kuleta mabadiliko na kuimarisha ustawi wa jamii.
Mara baada ya kushinda kwa jumla ya kura 423 katika mchakato ndani ya chama uliofanyika 27 mwezi wa nane katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 Mashavu ameonyesha uongozi wenye dira ya kuwainua wanawake na vijana wa Kigoma kwa kuacha alama mbalimbali ikiwemo kuwahamasisha wanawake kujiunga na siasa, kuhamasisha wanawake na vijana kujikwamua kiuchumi kwa kuanzisha miradi mbalimbali aidha amekuwa stari wa mbele kuwajengea uelewa wanaume kuruhusu wake zao kujiunga na siasa kazi aliyokuwa akiifanya tangu akiwa kiongozi wa chama, aidha kujitolea kwa kazi za kijamii zinazolenga kugusa Maisha ya kila mwananchi kila siku.
ALAMA ALIZOACHA
Akizungumza na THE PROFILE Mheshimiwa Mashavu ambaye ni mwanasiasa wa muda mrefu aliyeanza siasa tangu mwaka 1984 kama mjumbe wa kamati ya utekelezaji vijana ya chama cha Mapinduzi Mkoa wa Kigoma ambapo baadaye kuwa Katibu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya kwa zaidi ya miaka 20 na baadaye kuwa Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Kigoma mpaka mwaka 2022.
Aidha Mashavu amekuwa diwani kwa vipindi vitatu tofauti huku akiwa mshauri wa wanawake na vijana kama kiongozi,ambako kote alihakikisha sauti za wanawake na vijana zinawakilishwa kwenye vikao vya maamuzi na mipango ya maendeleo ya jamii inafikiwa kwa ufanisi.
UWEZESHAJI WANAWAKE, VIJANA
Akiwa Diwani wa Viti Maalum, Mashavu amejikita
katika kuwainua wanawake na vijana kiuchumi na kijamii. Ameandaa mikutano na
mafunzo kwa wanawake ili kuwasaidia kujiajiri na kupata maarifa ya
ujasiriamali. Aidha, ameshirikiana na wadau mbalimbali kuwapa vijana fursa za
kujifunza stadi za kazi na kujitegemea, pia ameshiriki katika kuwahamasisha
wanawake na mabinti kujiunga na siasa ili kuwawezesha kuwepo kwenye ngazi za
maamuzi.
UHURU ilipata fursa ya
kuongea na baadhi ya wananchi kuhusu mchango wa Diwani Mashavu katika Manispaa
ya Kigoma Ujiji kijana Malick Abdallah alisemaMashavu amekuwa na mchango mkubwa
kwa vijana kwani hutumia muda mwingi kutoa elimu na hamasa ya kujitegemea huku
akiwa mstari wa mbele kuhakikisha anasimamia asilimia 2 za mikopo ya vijana
ndani ya halmashauri.
“mama yetu huyu amekua
na mchango mkubwa kwa vijana hasa katika kuwahamasisha kujituma na kuhakikisha
wanajitegemea tunapenda kumuita bibi kwa kuwa anatusemea sana na kwa ukweli
tunampenda kwani mara kwa mara anatushauri vizuri anatuambia tulipotoka tulipo
na kama vijana tunapaswa kuwa na mchango gani katika jamii hakika ni mama
mwema” alisema Malick
AFYA NA USTAWI WA JAMII
Diwani Mashavu ameanzisha na kushiriki katika kampeni mbalimbali
za afya, ikiwa ni pamoja na kuhamasisha huduma za uzazi wa mpango, afya ya mama
na mtoto, na kutoa elimu ya kujikinga dhidi ya magonjwa yanayozuilika. Kupitia
juhudi hizi, amesaidia kuimarisha ustawi wa jamii hasa katika maeneo yenye
changamoto kubwa za kiafya.
CHANGAMOTO
Mheshimiwa Mashavu anasema licha ya umuhimu wa
mchango wa wanawake katika demokrasia, changamoto mbalimbali bado zinawakabili.
Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na mfumo dume unaochangiwa na mila na
desturi katika jamii nyingi ambazo zinawazuia wanawake kushiriki kikamilifu
kwenye siasa, jambo ambalo limewapa nafasi wanaume zaidi, Aidha Ukosefu wa
rasilimali fedha kumewafanya wanawake wengi wanakabiliwa na changamoto za
kiuchumi zinazowazuia kushindana na wanaume kisiasa.
"Ukosefu wa fedha za kuendesha kampeni,
pamoja na vikwazo vya kijamii kama kutokuwa na mitandao mizuri ya ushawishi,
vinawafanya wanawake kushindwa kupata nafasi za kisiasa,"anasema Mashavu.
FURSA ZILIZOPO
Mashavu anaiomba serikali na wadau
kusimamia sera, taratibu na sheria zilizopo kuhakikisha ushiriki wa wanawake
kwenye siasa unaongezeka huku akivitaka vyama kuhakikisha ilani zao zinawapa
nafasi wanawake na zinawalinda dhidi ya udhalilishaji wakati wa mchakato wa
uchaguzi ndani ya vyama ili kuondoa dhani porofu zilizojengwa tangu zamani.
"Jamii inapaswa kuelimishwa kuhusu umuhimu
wa wanawake katika uongozi, hii iendane na hamasa na kampeni kwa jamii kuhusu
faida za kuwa na wanawake kwenye uongozi, jamii inapaswa kuelewa kwamba haki
sawa katika siasa huchangia maendeleo na utawala bora,"anasema.
Aidha, anasema kutoa mafunzo na mitandao ya
uongozi ambapo wanawake wengi wanaweza kufaidika kwa kupata mafunzo ya uongozi
na msaada wa mitandao ya kisiasa, hatua ambayo itawawezesha kupata ujasiri na
maarifa ya kuongoza kwa ufanisi.
Diwani huyo anashauri kuwepo na mapambano juu ya
unyanyasaji wa kijinsia na kisaikolojia ni muhimu kuwepo sheria madhubuti za
kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia na kisaikolojia unaowalenga wanawake
katika siasa. hatua hizi zitasaidia kuondoa hofu na kuwahamasisha wanawake
wengi zaidi kushiriki kwani wapo viongozi wazuri wanaoweza ila wanakatishwa na
mfumo uliokuwepo.
MIPANGO YA BAADAYE
Diwani Mashavu ana mipango mingi yenye lengo la kuleta
mabadiliko ya kudumu kwa wakazi wa Kigoma Ujiji, kwa ushawishi alionao na
kwakushirikiana na madiwani wenzie anapanga kuimarisha miundombinu zaidi, hasa
katika sekta za afya na elimu, ili kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma
zenye viwango.
Aidha, ameazimia kuendelea kutoa mafunzo na kuwawezesha wanawake
na vijana kiuchumi, akilenga kuboresha maisha ya jamii nzima kwa ujumla.
Diwani Mashavu Juma Barakabitse amejitokeza kuwa mfano wa kuigwa katika uongozi
wa wanawake Mkoani Kigoma na nchini Tanzania. Mchango wake umekuwa na athari
kubwa kwa maendeleo ya Kigoma Ujiji, na kwa uongozi wake, jamii inapata mwanga
wa matumaini ya maendeleo endelevu. Ni muhimu kwa wananchi na wadau wengine
kuendelea kushirikiana naye ili kufanikisha malengo ya maendeleo ya jamii ya
Kigoma Ujiji.
VIONGOZI WENGINE WANAMSEMEAJE
“ Ndugu Mwandishi huyu
Diwani Mashavu kwetu sisi tunamuita dada kwanza ametutangulia kwenye siasa
lakini licha ya kutungangulia tu amekua shauri mzuri kwetu sisi viongozi
wanawake ametutia moyo na kutupa nguvu ya kuweza kufanya maendeleo amekua
mstari wa mbele kuwapigania wanawake kwa nguvu sana hasa kwa kuwatia ujasiri wa
kuhakikisha wanagombea nafasi za kisiasa lakini sio hivyo tu Diwani Mashavu ni
mama bora sit u kwa wanae bali hata kwa mabinti wengine ndani ya Jumuia ya
Wanawake Tnazania Mkoa wa Kigoma” alisema Mgeni Omary Kakolwa Naibu Mstahiki
Meya wa Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Pamoja na kuwa diwani Mashavu ni mke na mama wa
watoto 5. Na wajukuu 4 ambaye mbali ya kuwa kiongozi anashiriki katika ustawi
wa familia kwani arudipo nyumbani huandaa chakula kwa ajili ya familia yake
aidha Mashavu ni mfugaji wa mifugo mbalimbali ikiwemo n’gombe wa maziwa, mbuzi,
kondoo na kuku pia ni mkulima wa mazao mbalimbali ambayo huyatumia kuimarisha
ustawi wa familia yake.
WITO
Aidha, amewaasa wanasiasa na viongozi vijana
kushiriki katika ustawi wa familia bila kujali nafasi za uongozi walizo nazo
kwani kama viongozi wanapaswa kuwa mifano ya kuigwa kwa jamii inayowazunguka na
kuepukana na kasumba za sasa hivi zinazowataka haki sawa za kazi za nyumbani
kwa wanawake na wanaume amewataka wanawake na mabinti kuzingatia mila na
desturi za mtanzania ili kuwa mama bora.
"Demokrasia haiwezi kuwa kamili bila
ushiriki wa wanawake. Ingawa changamoto nyingi zinawakabili, kuna fursa nyingi
ambazo zinaweza kutumiwa kuhakikisha kwamba wanawake wanapata nafasi sawa
katika uongozi wa kisiasa. Kuongeza uwakilishi wa wanawake kutaboresha mchakato
wa kidemokrasia na kuleta maendeleo jumuishi kwa jamii. Ni jukumu la serikali,
vyama vya siasa, na jamii kwa ujumla kuhakikisha kuwa wanawake wanapewa nafasi
zinazostahili ili kuchangia katika ujenzi wa jamii bora,"anasema.
MWISHO
0 Maoni