Na Rose Mweko Geita
ASKOFU Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Kadinali Polycarp Pengo ametabaruku Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki la Geita ili kutoa fursa ya kanisa hilo kutumika tena baada ya uvamizi na uharibifu uliojitokeza.
Kadinali Pengo aliongoza ibaada ya kutabaruku kanisa hilo jana katika hafla iliyohudhuria na viongozi mbalimbali wa chama, serikali na madhehebu tofauti ikiwa na maana ya kuondoa kufuru iliyotendwa kwenye madhabahu ya kanisa hilo.
Akitoa salamu kwa niaba ya serikali, Mkuu wa Mkoa wa Geita Martin Shigella alisema baada ya kutokea kwa uvamizi huo, Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza ulinzi na usalama uimarishwe kwenye maeneo yote ya ibada.
Alisema pia Rais Dk Samia amesisitiza waumini wote bila kujali itikadi na dini zao wanedelee kushiriki kikamirifu kumwabudu mwenyezi Mungu kwani serikali itashiriki kuhakikisha kila mmoja anashiriki kikamirifu imani yake.
“Tunaendela kufuatilia, kuchunguza, na kubaini kama vipo viashiria vingine vilivyopelekea tukio hilo kutokea katika mkoa wetu.” Alisema na kuongeza;
“Nataka niwahakikishie waumini kwa niaba ya serikali, serikali inayoongozwa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan, ni serikali ambayo inaamini, inaheshimu, na inatii kwamba lazima tuzingatie misingi ya imani ya dini zetu.”
Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita, Flavian Kassalla aliishukuru serikali ya Rais Dk Samia Suluhu kwa ushirikino ilioutoa tangu uvamizi na uharibifu ulipofanyika ndani ya kanisa hilo mpaka kufanikisha ukarabati na kutabaruku kanisa.
Alisema ni vyema mamlaka za ulinzi na usalama zifanye uchunguzi wa kina kubaini kiini halisi cha tukio hilo kwani vipo viashiria vinavyoonyesha mtuhumiwa ni muumini wa kanisa hilo na alitenda kile anachokifahamu.
“Tuna mashaka sisi, kama mlevi tu anaweza kutenda aliyoyatenda, na ameyatenda kimkakati, kimpangilio, na kuhakikisha tunapata maumivu, tunaamini alikuwa na akiri zake timamu, na alinuwia, alikusudia na akatekeleza.
“Hii ni imani yetu, tunaomba sana, suala hili lifuatiliwe. Ikiwemo na maelezo yetu kama kanisa yatumike, ushahidi wetu tulioutoa, kwa sababu sisi tumekuwa mashahidi wa kwanza wa tukio na baadhi ya uharibifu tumeushuhudia.
“Tuna ushahidi mkubwa wa kwanza wa huyu mtu,baadhi ya matendo si ulevi tu, hata kama angekuwa amekunywa pombe, asingeweza kufanya, ikiwemo kitendo cha kuruka na kuvamia mtambo wetu wa kutunza kumbukumbu (CCTV).
“Mita mbili kwenda juu, awe na pepo, awe ni mtu tunadhani mwenye mafunzo makubwa, na mtatusamehe kwa kufikiria hivo, kwa hiyo kwetu sisi tunalitegemea jeshi la polisi, tusilipeleke suala hili haraka tutafute undani wake.”
Alisema Kanisa Katoliki lipo tayari kumsamehe mharifu huyoaachiwe huru ingali sababu ya kutenda tukio hilo itabainishwa ili kuhakiisha tukio kama hilo halijirudii na waamini wa kanisa katoliki waendelee kubakia salama.
Alisema hadi sasa takribani sh milioni 60 zimetumika kununua vifaa vipya vya ibaada kutoka nchini Italia na ukarabati wa maeneo mengine unaendelea.
Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya, Gervas Nyaisonga aliwaomba waamini wa Kanisa Katoliki jimbo katoliki la Geita na Tanzania nzima kutoteteleka kiiamni hata baada ya tukio hilo.
Awali Kadinali Pengo alisema baada ya tukio hilo waamini wa kanisa katoliki wanapaswa kutafakari Mwenyezi Mungu anatoa ujumbe gani na hivo wasimame imara katika imani, saran a toba ili kujiweka karibu na Mungu.
MWISHO
0 Maoni