NA ROSE MWEKO, GEITA
MTU asiyefahamika amevamia na kuingia ndani ya kanisa
Katoliki jimbo la Geita na kufanya uharibifu katika altare na sakrestia na
kuvunja tabernakulo huku akimwaga ekaristi takatifu na kuchana kitabu
kitakatifu Biblia huku akiharibu mfumo wa camera za ulinzi.
Taarifa iliyotolewa na Askofu wa Jimbo katoliki la Geita kwa
njia ya simu Flavian Matindi Kasalla amesema mtu huyo alivunja kioo cha
mlangoni na kuharibu madhabahu takatifu huku akiharibu sehemu mbalimbali za
ibada na kuharibu vitabu vitakatifu.
“mpaka sasa hatujajua alikotokea na wala hatujui aliingia
saa ngapi japo ilikua ni usiku wa kuamkia siku ya jumapili, kanisa letu
linalindwa na kampuni ya ulinzi ila mpaka sasa ni kitendawili kuwa mlinzi
alikuwa wapi, mtu aliyefanya tukio hilo amekamatwa na ameshafikishwa katika
vyombo vya usalama pamoja na mlinzi
aliyekuwa zamu siku hiyo” alisema Askofu Kasalla.
Watu wawili wanashilikiwa na jeshi la Polisi kwa mahojiano
zaidi akithibithisha kukamatwa kwa watu hao Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita
ACP Berthaneema Mlay alisema jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi zaidi ili
kubaini nani kamtuma na sababu za kufanya uharibifu huo.
“mtu huyo anaonekana alikuwa mlinzi na ni mtu ambaye amekuwa
akihudumu katika kanisani haswa huko alikotoka Bukoba hivyo jeshi la polisi
linaendelea na uchunguzi na itakapobainika tutatoa taarifa zaidi kwani mpaka sasa
kuna mambo tunayafuatilia tatutayazungumza ili kutovuruga upelelezi.
MWISHO
0 Maoni