Mkuu wa mkoa wa Kagera Albert Chalamila akigawa miche ya miti rafiki aina ya parachichi kwa wananchi Zoezi lililofanyika katika kata ya Kamagambo Wilayani Karagwe.
Na Angela Sebastian
Kagera
Mkuu wa mkoa wa Kagera Albert Chalamila amewataka wananchi wa mkoa wa Kagera kuendelea kuunga mkono juhudi za wawekezaji wanaowekeza katika nyanja mbalimbali za kuuletea mkoa huo maendeleo hususani Kampuni ya KADERES iliyoko Wilaya Karagwe mkoani humo inayojihusisha na utunzaji wa mazingira,mabadiliko ya tabianchi na kuondoa umaskini kwa wananchi na siyo kuwakatisha tamaa kwa kuwapiga majungu hari inayoweza kufifisha maendeleo.
Ametoa rai hiyo leo wakati akizindua mpango wa uvunaji wa hewa ukaa,utunzaji wa vyanzo vya maji na uhifadhi endelevu wa mazingira unaoendeshwa na Kaderes kwa udhamini wa banki ya kusaidia wakulima duniani iitwayo Rabo banki ya nchini Uholanzi .
"Kumekuwa na tabia wakati fulani ata kwetu viongozo wa Serikali kuwa pia hatuoni thamani ya wawekezaji binafsi katika kuhamasisha maendeleo ya Wilaya au mkoa inafika kipindi wawekezaji wanaweza kuwa na makosa kidogo tu lakini, watumishi wa Serikali wengine unakuta wamekaa kutegeshea kwenda kuomba rushwa na kukwamisha uwekezaji nimekuja kuonyesha thamani ya uwekezaji wa aina ya akina Kaderes kwani wakiungwa mkono matunda yao yataonekana kwa watu wengi"ameeleza Chalamila.
Aidha Chalamila amewataka wananchi kuendelea kutunza mazingira kwa kupanda miti mbalimbali,kufuga nyuki,kulima kilimo chenye tija ili waweze kupata faida kwa mara mbili ikiwemo mazingira pia kupata chakula na fedha za kujikimu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni ya Kaderes Leonard Kachebonaho amesema lengo la mradi huo ni kupambana na mabadiliko ya tabianchi, kuzuia mmomonyoko wa ardhi, utunzaji wa mazingira,kuongeza usalama wa chakula na kuwaunganisha wakulima wadogo na masoko ya Kimataifa ya hewa ukaa ambapo mpaka sasa wakulima 420 wamenufaika kutokana na mpango huo kwa kulipwa shilingi milioni 283 baada ya kuvuna hewa ukaa.
Amesema mradi huo unatarajiwa kudumu kwa kipindi cha miaka 20 kutokana na mkataba wao na Rebo banki ambapo wanatarajia kuwaingiza wakulima milioni 1.5 katika mradi ambapo mpaka sasa wameweza kusaiiri wakulima 42,000 na wanatarajia kufikia wakulima laki moja mwishoni mwa mwaka huu.
Naye mmoja wa wakulima wanaoendelea kunufaika na mpango huo Richard Banyamulana anasema miaka miwili iliyopoita wakati Kaderes ikipita na kutoa elimu na hamasa kwa wakulima wapande miti rafiki wakulima hao waliona kama utani lakini hivi sasa amelipwa zaidi ya shil. Mil.1.6 kutokana na kufanyiwa tathimini ya kuvuna hewa ukaa ambapo pesa hiyo imemsaidia kulipa ada za shule kwa.watoto wake,kununua ng'ombe mloja wa maziwa na kuongeza lishe kwa familia yake.
MWISHO.
0 Maoni