JESHI la Polisi mkoani Geita limethibitisha kifo cha mchungaji, Abdiel Raphael (42) mkazi wa mtaa wa Uwanja kata ya Nyankumbu mjini Geita aliyefariki akiwa katika maombi na mfungo wa siku nane.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Safia Jongo alitoa taarifa hiyo jana alipozungumuza na waandishi wa habari na kueleza mchungaji huyo alikutwa na umauti Desemba 3, 2022 akiwa ndani kwake.
Alisema marehemu alikuwa na kanisa nyumbani kwake na wakati akiingia katika maombi na mfungo aliwaaminisha waumini wake endapo wataona amefariki wasiwe na shaka kwani atafufuka.
“Mpaka ailipofika tarehe nane wanaendelea na maombi lakini akawa hafufuki, ilipofika tarehe 9, na ile hali ya mwili kuendelea kuharibika, ndipo walipoamua kutoa taarifa kwa mwemnyekiti wa mtaa.
“Na kweli madaktari walipomfanyia uchunguzi wakakuta huyu mtu alikuwa ameshakufa kwa siku nyingi sana, na alivyofanyiwa uchunguzi akakutwa chanzo cha kifo chake ni kutokula kwa muda mrefu.
“Alikuwa anawaaminisha waumini wake kwamba anao uwezo wa kufa na kufufuka, anao uwezo wa kuishi bila kula kama Yesu (kristo) na bado akafa na akafufuka.”
Kamanda alisema nyumba hiyo ambayo marehemu alikutwa amefariki ilikuwa ni nyumba ya kupanga, na alikuwa anafanya uchungaji wa binafsi na dhehebu lake halijafahamika.
Kamanda aliwaomba wananchi kuwa makini na kutoingia katika mkumbo wa madhehebu yanayoendelea kuibuka na wasije kujikuta katika imani ambazo zinawza kupelekea taharuki.
Mjumbe wa serikali ya mtaa wa Uwanja, Jumanne Zuberi alikiri tukio hilo kuibua taharuki mtaani hapo ambayo ilitokana na harufu ya mwili wa mchungaji huyo ambaye alianza mfungo wake Novemba 28.
Mwenyekiti wa mtaa Uwanja, Enos Cherehani alisema kabla ya kukutwa na umauti mchungaji huyo aligeuka kero mtaani hapo kwa kutotaka familia yake kuchangamana na majirani ili waiharibiwe imani.
mwisho
0 Maoni