NA ROSE MWEKO, GEITA
JESHI la Polisi mkoani Geita linamushikikilia Oliver Meshack (19) mkazi wa kitongoji cha Mapinduzi, kata ya Buselesele wilayani Chato kwa tuhuma za kumuzika mwanaye akiwa hai ili apate nafasi ya kufanya biashara ya ngono (kudanga).
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Safia Jongo ametoa taarifa hiyo jana alipozungumuza na waandishi wa habari ofisini kwake na kumtaja mtoto aliyezikwa alijulikana kwa jina moja la Queen akiwa na umri wa wiki mbili.
Kamanda alisema mtuhumiwa alitenda ukatili huo Desemba 2, 2022 majira ya saa nane usiku ambapo taarifa zilifikishwa kituo cha polisi Desemba 6 na wananchi walidai kushangazwa na kupotea ghafla kwa kichanga huyo.
“Walisema wanajua kuna binti amejifungua mtoto, lakini wana siku zaidi ya tatu hawamuoni huyu binti akiwa na huyo mtoto, kwa hiyo wana wasiwasi na wanatamani wajue huyo binti amepeleka wapi huyo mtoto.
“Jeshi la polisi lilimuchukua huyo binti na kufanya naye mahojiano, ambapo alikiri kwamba ni kweli alijifungua huyo mtoto ambaye alimuzika akiwa na umri wa wiki mbili.” Alisema na kuongeza,
“Kutokana na yeye kazi yake ni kuuza baa na pia ananjiuza mwili wake, kwa hiyo yule mtoto akawa ni kero kwake, akawa anashindwa kwenda kufanya biashara yake hivo akaamua kuchimba shimo, na kumfukia huyo mtoto akiwa hai.”
Alisema binti aliwaongoza maofisa wa polisi mpaka eneo alipomuzika mwanaye na kisha kufukua ambapo walikuta tayari mtoto ameshafariki na mwili ulikabidhiwa kwa taratibu zingine za mazishi.
“Hiki ni kitendo kibaya, ni kitendo cha kikatili sana, na mbaya zaidi kilitokea kipindi hiki cha siku 16 za kupinga ukatili, na huo ni miongoni mwa ukatili ambao ulitokea.”
Kamanda Safia alisema katika kipindi hiki binti huyo ametafutiwa wanasaikolojia kuendelea kumpatia tiba ya afya ya akili huku aliyaomba mashirika yasiyo ya kiserikali kuwasaidia mabinti wengine kama hao.
MWISHO
0 Maoni