MKURUGENZI WA HALMASHAURI YA WILAYA YA GEITA JOHN WANGA AKIKABIDHI VITANDA 20 VYA WAGONJWA KITUO CHA AFYA KATORO

Na Rose Mweko, Geita.

MKURUGENZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Paul Wanga amesema Halmashauri ya Geita imeanza kuchukua hatua madhubuti ya kuhakikisha inamaliza kero ya uhaba wa vitanda vya wagonjwa kwenye vituo vya afya.

Wanga amesema hayo jana mara baada ya kukabidhi vitanda vya wagonjwa 20 katika kituo cha afya cha Katoro ambacho kilichokuwa na uhaba wa uhaba wa vitanda, jambo ambalo litasaidia kupunguza changamoto hiyo.

 

JOHN WANGA AKIKABIDHI VITANDA NA GODORO KITUO CHA AFYA KATORO

Alisema mpango huo unalenga kuwezesha vituo vya afya kumudu idadi kubwa ya wagonjwa hasa kina mama na wanaofika kupata huduma ambapo mpaka sasa kituo cha afya Katoro kinahudumia kina mama wazazi kati ya 30 hadi 40 kwa siku.

 “Hii ni sehemu tu ya vitanda ambavyo tumeagiza, jumla tumeagiza vitanda 50, kwa hiyo tumeanza na 20 hivi ambavyo ndio vimefika tumevipokea, na kwa hiyo tunavileta hapa kituoni kwa ajili ya kuvikabidhi sasa.

 


“Sisi kama Halmashauri ya Wilaya ya Geita tunaendelea kukamilisha hospitali yenye hadhi ya wilaya iliyopo Katoro (mji mdogo), ianze kufanya kazi, ambapo tunatarajia kati ya mwezi Januari  2023 hospitali hiyo ianze kutoa huduma.

 “Kwa hiyo tutapunguza msongamano mkubwa katika kituo hiki cha afya (Katoro) na wengi sasa wataenda kuhudumiwa kwenye hiyo hospitali yenye hadhi ya wilaya.” Alieleza Wanga.

 


Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Dk Modest Burchard alibainisha vitanda 20 vya wagonjwa vimegharimu Sh milioni 14 ambapo vimeongeza idadi katika kituo cha afya Katoro kutoka vitanda 66 hadi vitanda 86.

 Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Katoro, Dk Zakayo Sungura alisema vitanda hivyo vitaondoa tatizo la kina mama kulala wawili kwenye kitanda kimoja baada ya kujifungua na hivyo itasaidia kuweka mazingira rafiki ya kutoa huduma.

 



“Kituo chetu cha afya kimekuwa kikipata wazazi kwa mwezi wanaojifungua takribani 900 mpaka 1000 kwa miezi mitatu mfululizo, lakini hali hii huwa siyo ya kudumu kuna kipindi wanajifungua 600, 700 mpaka 800.”alisema Sungura. 

MWISHO.