WAZIRI SELEMANI JAFO AKIPATA UFAFANUZI WA MKAA MBADALA KUTOKA KWA MENEJA MASOKO NA MAHUSIANO WA STAMICO GEOFREY MEENA KATIKA BANDA LA MAONESHO YA TEKNOLOJIA YA MADINI GEITA. 

Na Rose Mweko , GEITA

Shirika la Madini Nchini (STAMICO) limesema litaibeba agenda ya kutunza mazingira nchini kwa kutengeneza mkaa mbadala kwa wingi ili kuzuia ukataji wa miti unaofanyika nchini ili kupata nishati ya kupikia aina ya mkaa wa kawaida.



Aidha STAMICO imesema inakusudia kujenga viwanda viwili vikubwa vya kutengeneza mkaa mbadala eneo la Kibaha mkoani Pwani na Kiwira kwa kufunga mitambo ya kisasa ya kuzalisha mkaa huo vyenye uwezo wa kuzalisha tani elfu 20 kwa saa kila kimoja.

Meneja wa Masoko na Mawasiliano wa STAMICO Bw Godfrey Meena alimweleza Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais anae shughulikia Mazingira Dkt Suleiman Jafo wakati alipofanya ziara ya kutembelea maonesho ya 5 ya kitaifa ya teknolojia ya madini na uwekezaji mkoani Geita.


"Mbali na STAMICO kuwa na jukumu la kuwalea wachimbaji wadogo ili wakue wawe wa ngazi ya kati hadi wakubwa, tunalo pia jukumu la kutunza mazingira kwa kupanda miti katika maeneo yanapofanyika machimbo ya madini lakini pia kwa kutumia utaalam mwingine wa kutengeneza mashimo ya kuingilia migodini badala ya kutumia miti" alisema Meneja Masoko Bw Meena.


Nae Afisa Mwandamizi anae shughulikia Usalama maeneo ya migodi katika mgodi unao milikiwa na STAMICO wilayani Biharamulo mkoani Kagera wa STAMIGOLD Bw Fred Makwebeta amemkaribisha Waziri wa Mazingira Mhe Dkt  Suleiman Jafo kutembelea mgodi wa STAMIGOLD uliopo Biharamulo ili kujionea jinsi STAMIGOLD inavyo tunza mazingira na kuokoa ukataji miti.


Waziri Dkt Jafo amepongeza juhudi kubwa na nzuri zinazofanywa na STAMICO katika agenda ya kutunza mazingira hapa nchini na kuwataka STAMIGOLD kutengeneza mkaa mbadala wa kutosha kukidhi mahitaji ya nishati mbadala nchini.

Halikadhali Dkt Jafo  amewataka STAMIGOLD kuvitumia vikundi vya akina mama kwa kuwawezesha kufunga mitambo kila Halmashauri ili watengeneze mkaa mbadala wa kutosha na kufanya wakala wa misitu nchini (TFS) kupunguza utoaji vibali vya kukata miti kwa ajili ya kutengeneza mkaa jambo ambalo amesema linachangia uharibifu wa mazingira ulio mkubwa.

Awali Meneja wa Masoko na Mawasiliano  wa STAMICO Bw Godfrey Meena alimweleza Waziri wa Mazingira Mhe Dkt Suleiman Jafo kwamba STAMICO imepanga kupanda miti Elfu 10 kwa kuanzia mkoa wa Dodoma hadi kuja mpaka mkoani Geita.

Kwa sasa STAMICO ipo kwenye kampeni ya kuutangaza mkaa mbadala inao utengeneza kutoka STAMIGOLD unaoitwa "Rafiki Briquettes" ambao una nguvu mara tatu ya mkaa wa kawaida na unauzwa kilo moja kwa shilingi elfu moja katika maonesho ya 5 ya kitaifa ya teknolojia ya madini na uwekezaji yanayo endelea mjini Geita.