RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AKIWA  MJI MDOGO WAKATORO MKOANI GEITA.

Na Rose Mweko ,Geita 
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu amesema mpango wa bima ya afya.kwa wote ni mkombozi wa wananchi hivyo wanapaswa wajiandae kuupokea kwani ni suluhisho kwani utawasaidia pale watakapopatwa na maradhi.


Rais Samia amesema hayo jana wilayani Chato baada ya kutembelea na  kukagua hospital ya rufaa ya kanda ya chato na kuridhishwa na maendeleo yake.

Alisema  mpango wa bima ya afya kwa wote unalengo la kuboresha huduma za matibabu nchini na hivyo kuviwezesha hospitali na vituo vya afya kuboresha huduma kuwa za uhakika na haraka tofauti na ilivyo sasa.

“Niwaombe sana tutakapokuja na mfumo wa bima ya afya kwa wote, wote tukanunue bima, ni kupitia bima hizo, tunaweza tukaboresha zaidi na zaidi huduma za afya” Alisistiza Rais Samia.

BAADHI YA VIFAA VYA HOSPITAL  VILIVYOKO KATIKA HOSPITALI YA RUFAA YA KANDA YA CHATO.

Aidha Rais Samia aliwahahakishia wakazi wa Chato, Geita na nchi nzima atahakikisha mradi wa Ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda chato unakamilika kama ilivyopangwa ili kusogeza huduma za kibingwa.

“Nitaijenga kama ilivyokusudiwa, wataalamu wa kutosha tumeshaleta na tutaendelea kuleta, ndani ya hospitali hii kuna vifaa vya kisasa kabisa kuchukua vipimo vyote, ambapo mwanzo ilibidi muende Bugando, sasa vipimo vyote vitachukuliwa hapa.” Alieleza.

Akitoa taarifa ya mradi wa ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya kanda Chato, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Daudi Kondoro alisema awamu ya kwanza ya ujenzi imekamika kwa asilimia 99.

WANANCHI WA MJI MDOGO WA KATORO WAKIMSIKILIZA  RAIS SAMIA 

Alisema awamu ya kwanza imegharimu Sh bilioni 13 na imehusisha Jengo la Wagonjwa wa Nje (OPD), Duka la Dawa, Jengo la Wagonjwa wa Dharura na Jengo la Wagonjwa wa Uangalizi wa Karibu (ICU).

Alisema awamu ya pili ya ujenzi itagharimu Sh bilioni 18.5 na serikali imeshatoa Sh bilioni 12.8 kwa ajili ya jengo la mionzi ambalo limeshakamilika na wodi ya kuchukua vitanda 210 na imefikia asilimia 65.

Alisema awamu ya tatu ya ujenzi itahusisha ujenzi wa jengo la mama na mtoto, jengo la kuhifadhia maiti pamoja na jengo la kufulia na tayari wameshatenga maeneo rasmi kwa ajili ya kujenga majengo hayo.

Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato, Dk Bryan Mawala alisema hospitali ilianza kutoa huduma Julai 30, 2021 na sasa imehudumia takribani wagonjwa 15,000 kati yao wagonjwa wa ndani 3,450.



Dk Mawala alibainisha hospitali ilianza na watumishi 79 na baadaye kuongezewa watumishi 39 na kisha watumishi wengine 88 na mpaka sasa hospitali ina jumla ya watumishi wa afya 206.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella alisema wamepokea Sh bilioni tatu kutoka kwenye fedha za tozo ambazo  zimewezesha ujenzi wa vituo vya afya sita na tayari vimeshaanza kutoa huduma za awali.

Aidha Rais Samia alipokua safarini kuelekea mjini Geita alipata wasaa wa kuwasalimia wananchi wa Buseresere- Katoro ambapo alisema zaidi ya shilingi billion 15 zimeletwa mkoani Geita ili kukamilisha mradi wa maji kutoka kijiji cha Chankolonko na kusambazwa katika mji wa Katoro-Buseresere na  vijiji vya jirani.
"Kupitia wakala wa barabara vijijini tutaendelea kufungua barabara za vijijini na mitaa na ninawaahidi tutafunga taa za barabarani ili kuhakikisha mji wetu unakuwa safi hata hivyo ninatarajia kufanya mengi hata hivyo maendeleo ni hatua hivyo tuwe wavumilivu, mimi hapa Geita ni nyumbani", alisema Rais Samia Suluhu Hassan. 

MWISHO