KAMANDA WA POLISI MKOA WA GEITA SACP LEONARD MWAIBAMBE |
KUPOROMOKA KWA MAADILI KUNAWEZA KUSABABISHA UKATILI
NA MAUAJI
NA ROSE MWEKO, GEITA
UKATILI wa kijinsia ni ukatili unaofanyika kwa
binadamu ukihusisha vitu mbalimbali ikiwemo ukatili wa kisaikolojia ukatili wa
kudhuru mwili kujeruhi na kuua.
Hivi karibuni katika Mkoa wa Geita kumekuwepo na
matukio mengi yanayohusisha ukatili ikiwemo watu kuua na kujiua kwa sababu
mbalimbali jambo lililoilazimu Serikali ya Mkoa kuwaita viongozi wa dini ili
kujadiliana mambo mbalimbali ikiwemo masuala hayo yanayohusu mauaji kwani
mauaji mengi yametokea yakihusisha mapenzi, imani za kishirikina na msongo wa
mawazo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita SACP Leonard
Mwaibambe katika kikao chake na viongozi wa dini alisema kama viongozi wa dini
watashirikiana na Serikali katika kuhakikisha inatokomeza vitendo vya ukatili
basi ni imanii ya serikali kuwa vitendo hivyo vitakoma kwani viongozi hao
wanamchango mkubwa katika kuakikisha wanawaponya waumini wao kiimani na
kisaikolojia.
Alisema chanzo cha matukio hayo ni mmomonyoko wa
maadili ambapo Serikali iliomba viongozi wa dini waingilie kati kwani matukio
ya kubaka haswa kwa wazazi kuwabaka watoto wao chuki na visasi visivyoelezeka
na ukizingatia Mkoa wa Geita ulikuwa na sifa mbaya ya mauaji yaliyochochewa
na imani za kishirikina.
“ matukio mengi ya watu kujiua yanatokana na msongo wa mawazo na mauaji haya yametokea ndani ya miezi saba mfululizo tofauti na ilivyooelezewa na wanahabari na kufanya ionekane kuwa matukio yote yanaonekana yamefanyika kwa mwaka huu pekee, niliamua kuwaita viongozi wa dini na kuwaeleza matukio ya mauaji yalivyo ili kuionyesha jamii kuwa kuna haja ya viongozi wa dini kuingilia kati jambo hili ili kwa pamoja tuweze kutafuta suluhu ya jambo hili na kama ni suala la kiimani lishughulikiwe kiimani lakini kama ni tatizo la kisaikolojia tuweze kushirikiana kuhakikisha tunatatua matatizo haya kisaikolojia hii itasaidia kupunguza matukio haya ambayo kwa kiasi kikubwa yamekuwa mengi” alisema Kamanda Mwaibambe.
Aidha matukio mengine yanatokea lakini chanzo chake
ni msongo wa mawazo unaosababishwa na wazazi na jamii inayowazunguka walengwa
kwani katika matukio hayo kuna tukio lililovuta hisia za watu la binti wa miaka
17 kujinyonga baada ya kuachika mara tatu.
“ katika tukio kama hilo la binti wa miaka 17
kujinyonga lilihusishwa na wazazi kuendekeza tamaa ya mali na kuwashinikiza
watoto wao kuolewa ndoa za utotoni katika hali ya kawaida binti wa miaka 17
kuwa amekwisha kuolewa mara tatu ina maana ndoa yake ya kwanza aliolewa akiwa
na umri wa miaka mingapii? Inawezekana ikawa chini ya miaka 15, Alihoji Kamanda
Mwaibambe, alisema binti huyo inaelekea alikuwa na ndoto zake za kusoma na
kujiendeleza kimaisha na alipokatishwa kusoma na kwenda kuolewa ndipo alipoanza
kukosa uelekeo wa maisha na hivyo kupata msongo wa mawazo kwani kwa wakati huo
jamii na wazazi wa jamii yake wanaonelea kwamba maisha ni ndoa na si vinginevyo”
Alisema Mwaibambe.
Aidha mfumo dume kwa makabila ya kanda ya ziwa
unasababisha kuwatenga akina mama na haki zozote juu yao hata haki zao wenyewe
kama kuachishwa masomo na kulazimisha kuolewa nap engine mtoto wa kike
kufanyiwa ukatili wa kingono kama kubakwa lakini badala ya jambo hilo
kuripotiwa katika vyombo vya dola wazazi na walezi hukubaliana na mbakaji na
kulipa fidia ndogo ambayo kwanza haimfikii mlengwa lakini pia haiondoi jeraha
la ukatili alilofanyiwa muhusika hivyo vitendo kama hivi mara nyingi
husababisha matokeo mengi ya kujidhuru na kudhuru wengine kwakua mtendewa
anakuwa hana sehemu ya kukimbilia na kupeleka malalamiko yake.
Hali kama hiyo ndio huzaa matokeo kama yale ya
tarehe 1 desemba 2021 ambapo mwanamke mmoja ajulikanae kwa jina la Veronica
Gabriel mkazi wa Mwabagaluka kata ya Buseresere alikunywa sumu na kuwanywesha
sumu watoto wake watano huku akidai kuwa kaamua kufikia maamuzi hayo kutokana
na ugumu wa maisha.
“hii si hali ya kawaida kwa mtu kufikia hatua hii hivyo kama Jeshi la Polisi ndio maana tukafikia hatua ya kuwaita na kuaa na viongozi wa dini ili waweze kukaa na waumini wao kuzungumza juu ya mambo ya dini na imani aidha kuiasa jamii kuacha kuwatenga watu wanaopatwa na changamoto za maisha kwani kwa kuwatenga mbali nao husababisha msongo wa mawazo na kufikia hatua kama hii ambayo ni hatua ya mwisho ya kukata tama” alisema Mwaibambe.
THE PROFILE BLOG iliwatafuta viongozi wa dini kupitia Jumuiya ya Maridhiano Tanzania Mkoa wa Geita kuzungumzia suala la ukatili wa aina mbalimbali na mikakati ya viongozi hao kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa wa Geita namna ya kutokomeza ambapo Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Alhadi Kabaju Shekhe wa Mkoa wa Geita alisema kazi ya viongozi wa dini ni kuwahubiria wananchi habari njema za Mungu na kuwatoa katika kukata tamaa kwani chanzo cha mauaji mengi ni msongo wa mawazo na kukata tamaa hivyo kwa umoja wao katika nyumba za ibada umewekwa mkakati wa kuhakikisha waumini wanahubiriwa maneno ya Mungu.
“licha ya kujidhuru au kudhuru wengine kitendo cha
mauaji ni dhambi na mtu aliyejiua hana nafasi peponi, vitabu vya dini vinasema
mtu aliyejiua anakwenda moja kwa moja jehanamu hivyo kujiua sio suluhisho la
matatizo uliyonayo na kwamba itafutwe njia mbadala wa kuhakikisha unatatua
changamoto uliyonayo,aidha sisi kama viongozi wa dini tumekubaliana kuelimisha
jamii kuondokana na mfumo dume kandamizi unaopelekea wanawake kukosa haki zao
hasa zile haki zao binafsi kwa mfano
kitendo cha yule dada aliyejiua kwa kuwa kaachika ndoa tatu huku akiwa na umri
wa miaka 17 ni kielelezo tosha kuwa huyu binti aliolewa ndoa za utotoni ndio
maana katika umri wa miaka 17 kaachika mara tatu na kwamba baada ya kukatishwa
ndoto alizokuwa nazo hakuna jambo analoliwaza zaidi ya kuolewa ndio maana
alipoona hawezi kumudu kuolewa alichukua maamuzi ya kujiua jambo ambalo kiiman
na kibinadamu halifai” alisema Shekhe Alhadi.
Naye katibu wa Jumuiya hiyo ya maridhiano mchungaji
Joshua William alisema wao kama viongozi wa dini kazi yao ni kuponya roho
zinazoonekana kukata tamaa na kujiingiza katika mambo yasiyompendeza Mungu na
katika mikakati waliyojiwekea ni pamoja na kutokomeza ukatili wa aina
mbalimbali kwani vyote hivyo ni chukizo mbele za Mungu na matukio yote haya hufanywa
kwakuwa tu maadili ya neno la Mungu hayapo miayoni mwao.
“ushauri wangu kwa jamii tumtafute Mungu misikiti
ipo makanisa yapo hata sisi viongozi wa dini tupo muda wote kuhakikisha
tunashauri na kukuongoza muumini katika kulijua nenoo lake ili kukuepusha na
aina yoyote ya kufikiria kutenda dhambi, aidha maombi ni silaha ya kila jambo
hivyo niwaombe jamii tusiache kusali na kuendekeza kazi na starehe za dunia
tujipe muda wa kuutafuta uso wa Mungu hakika nawahakikishia mambo mengi
yatafunguka na utamtukuza Mungu” alisema Mchungaji Willium.
Baadhi ya wananchi wametoa maoni yao kuhusu matokeo ya ukatili na matukio ya
kujiua ambapo Alfred Mabuga Sekule
alisema kujiua ni matokeo ya mambo mengi yanayotokea katika jamii kubwa
ikiwa ni Mmomonyoko wa madili na
imani ya ki Mungu kwani katika kipindi cha karibuni watu wengi wameanza
kushuka ki imani na hii kupelekea mtu kushawishika kutenda uharifu maana yake
ubinadamu na hali ya undugu umepungua.
“Mila na desturi baadhi ya maeneo bado wanaamini kuwa bibi akiwa na macho mekundu ni mchwawi,mtu akituhumiwa kwa jambo fulani bila ushahidi kijijini basi mtu huyo hufukuzwa kijijini na kutengwa kabisa na wakati mwingine kuuwawa bila hatia haya yote ni matokeo ya ukatili na chanzo chake ikiwa ni kukosekana kwa elimu ya neno la Mungu na wakati mwingine mila na desturi kandamizi, sababu ya haya wakati mwingine viongozi wa dini wameanza kuchanganya siasa na dini na kusahau nafasi yao katika jamii, wakati jamii ikimtegemea kiongozi wa dini kuwahubiria watu habari njema siku hizi kumeibuka kwa viongozi wa dini wanaokuwa mashabiki wa kisiasa hivyo wananchi kukosa chakula cha kiroho” alisema Mabuga.
Aidha Mabuga alisema Imani za kishirikina hasa katika maeneo ya machimboni imeshika kasi sana na hii kupelekea mauaji ya ndugu zetu ulemavu wa ngozi, ubakaji kwa watoto hasa watoto wetu wenyewe na matukio mengi ya kihalifu lakini msingi wa haya yote ni kukosekana kwa elimu ya dini na watu kutokuwa na hofu ya Mungu.
“tunaomba Serikali ifike mahali itilie mkazo suala hili la imani ya kupata utajiri kwa kutumia viungo vya binadamu, hivi karibuni huko Mkoani Simiyu kauwawa mtu mwenye ulemavu wa ngozi na katika matukio mengine tumesikia kwenye vyombo vya habari sehemu tofautitofauti tumesikia watu wameanza tabia ya kufukua makaburi kwa imani ya kupata mali jambo hili si utamaduni wa mtanzania hii ni taa inayoashiria kumomonyoka kwa maadili na kuporomoka kwa utu wetu ambao ndio ilikua jambo la kujivunia” alisema Mabuga.
Aidha sababu nyingine ni kukua kwa Sayansi na teknolojia ambapo utandawazi sasa umeonekana kuwa tishio kwa maadili mila n desturi za Mtanzania kwani kutokana na watu kujikita sana katika mambo ya utandawazi tayari athari mbalimbali zimeanza kujitokeza ikiwemo kupungua kwa umoja, upendo na mshikamano, nidhamu na ushirikiano ambao watanzania walijivunia utandawazi umeyavunja na kuathiri kwa kwang kikubwa tamaduni kama watanzania .
Mwalimu Mariam
Nyabakari ni mzazi na mlezi alisema jamii ya sasa kama haitakazaniwa na
kurudishwa katika maadili yale ya mwanzo kuna tishio la kupata kizazi
kilichohatarishi zaidi kwani watanzania wameanza kulea kizazi legelege kwa jina
la kuwapenda watoto wao.
Alisema hapo zamani
ilikuwa watoto wanapofika shuleni hufundishwa masomo na stadi za kazi ikiwemo
kulima kupika na mengine mengi hii ilimjenga mtoto katika kutambua majukumu
yake atakapokuwa aidha kama mtoto atafanya makosa walimu walitoa adhabu ya
viboko na adhabu nyingine kama kumkanya mtoto aachane na tabia hiyo
isiyoridhisha lakini siku hizi kama itatokea mwalimu atamuadhibu mtoto basi
wazazi na walezi wanakuja juu na wakati mwingine mwalimu anaweza pata
misukosuko jambo ambalo walimu wengi siku hizi huamua kujiepusha nalo na
kuwaacha watoto wafanye wanachojisikia jamboo ambalo ni hatari kwa jamii.
“kutokana na malezi tunayowaacha watoto wetu siku hizi ya kuwawekea wafanyakazi na kutotaka watoto wafanye kazi sasa tunazalisha kizazi cha watu wavivu na goigoi ambao hawataweza hata kujimudu wenyewe na matokeo yake hujiingiza katika vitendo vya kihalifu kwa matarajio ya kupata mahitaji yao kwa njia ya mkato na ikitokea wakashindwa kupata ndipo huingia katika ukatili ama wa kuwadguru wengine au kujidhuru kwa sababu mtoto hakufundishwa kujitegemea tokea aiwa mdogo” alisema Mwalimu Nyabakari.
Aidha ukiukwaji wa maadili ya kazi sehemu za maamuzi hasa rushwa , umesababisha watu kuwa na visasi na hasira na hatimaye kujichukulia sheria mkononi kwa kuua,kuvunja,kuchoma vitu au hata kujiua wenyewe au hata hasira kuipeleka nyumbani kwa watoto,mke au mume na hivyo kusababisha matokeo mabaya zaidi hivyo tuwaombe viongozi na jamii kushirikiana katika kuhakikisha mambo haya na matukio ya kihalifu yanatokomezwa.
MWISHO
0 Maoni